Uingereza, Ufaransa, Uholanzi na Uhispania zinachuana kutinga fainali ya Euro 2024 |
Timu nne zinajiandaa kwa nusu fainali ya Euro 2024, Uhispania kumenyana na Ufaransa siku ya Jumanne huku Uingereza ikimenyana na Uholanzi siku inayofuata.
Uhispania wanatafuta kushinda kombe hilo kwa mara ya nne, baada ya kushinda mara ya mwisho mwaka 2012.
Ufaransa ilishinda mara ya mwisho miaka 24 iliyopita, huku Waholanzi wakitwaa ubingwa mwaka 1988 - na bila shaka Uingereza ina matumaini ya kushinda kwa mara ya kwanza kombe la mataifa ya Ulaya.
BBC Sport iliwauliza wataalamu wa soka kutoka kila nchi kuhusu maoni yao:
Uhispania ilicheza mchezo mgumu dhidi ya Ujerumani na kutinga nusu fainali |
Mwandishi wa michezo wa Uhispania Guillem Balague:
Kucheza dhidi ya Ufaransa itabidi tuwe na mipango, kama tulivyolazimika kuwa na mipango dhidi ya Italia, Albania na Georgia.
Itabidi tuwe waangalifu dhidi ya mashambulizi ya kushtukiza, kama tulivyofanya dhidi ya wapinzani wetu wote. Sisi ni wazuri katika kuzuia, ingawa tunafanya idadi kubwa ya makosa ya kimbinu.
Itakuwa muhimu kuwa makini katika mchezo mzima, huku wakiendelea kutafuta nafasi kupitia wachezaji wao wa mbele. Tutalazimika kuwa waangalifu dhidi ya kasi ya Ousmane Dembele na Kylian Mbappe.
Kwa sababu tunashambulia mara kwa mara, na kupiga mashuti na kutengeneza nafasi, tunaweza kuivunja safu yao ya ulinzi na kushinda dhidi ya Ufaransa.
Nadhani tutaifunga Ufaransa na tutakutana na England kwenye fainali. Anaona washindi ni Uhispania.
Uingereza ilipitia kwa mikwaju ya penalti na kuishinda Switzerland na kutinga hatua ya nne bora |
Mwandishi wa kandanda wa BBC, Phil McNulty:
England lazima itumie uwezo ulioonyeshwa na Jude Bellingham na Bukayo Saka ambao umewaweka kwenye nusu fainali baada ya kuwafunga Switzerland.
Kikosi cha Gareth Southgate kimepata tabu katika mechi za nyuma. Lakini mbinu ya kushambulia zaidi ya Uholanzi inaweza kuwapa wachezaji wabunifu wa England nafasi zaidi ya kufunga magoli.
England itahitaji kuwa katika kiwango bora zaidi katika safu yao ya ulinzi kwa sababu Waholanzi ni tishio kubwa katika safu ya ushambuliaji, Cody Gakpo wa Liverpool anacheza vizuri na Memphis Depay ni hatari.
Iwapo England watafanya vizuri wanaweza kuisumbua safu ya ulinzi ya Uholanzi ambayo inaonekana kuwa dhaifu.
Nahodha Harry Kane alitatizika sana kwenye robo fainali ya England dhidi ya Sweden, akionekana kuwa mfupi na asiye na kasi.
England wako katika mbio za kutaka kushinda Euro 2024. Wamefika nusu fainali mara kadhaa - fikiria Ugiriki mwaka 2004 na Ureno mwaka 2016.
Iwapo Uingereza itashinda taji lao la kwanza la Kombe la Mataifa ya Ulaya, haitanishangaza - wakati hisia zinasema ni Uingereza, kichwa kinasema Uhispania.
Uhispania wameonekana kuwa timu bora katika michuano ya Euro 2024, ingawa bado wanaweza kukwama dhidi ya Ufaransa yenye vipaji vikubwa chini ya Didier Deschamps.
Uhispania wana mchanganyiko mzuri wa vijana wenye uzoefu na wameonekana kuwa na timu ya kuvutia zaidi tangu mwanzo - lakini ninaamini watalazimika kuifunga England ili kushinda Euro 2024.
Kylian Mbappe amefunga bao moja hadi sasa kwenye Euro 2024 - penalti dhidi ya Poland katika hatua ya makundi |
Mwandishi wa habari wa soka wa Ufaransa Julien Laurens:
Tumeona ubora wa Ufaransa katika kujilinda. Huo ndio mtindo wao. Lakini wamekuwa na changamoto katika suala la kutengeneza nafasi.
Pamoja na Cristiano Ronaldo, Kylian Mbappe nae huenda akawa amekatishwa tamaa zaidi kwenye michuano hii.
Kwanza ni kwa sababu ya kinyago ambacho amelazimika kuvaa baada ya kuvunjika pua dhidi ya Austria. Katika mchezo huo alionekana mkali sana.
Pia alikuwa na masuala machache ya utimamu wa mwili kabla ya Euro, kwa hivyo sidhani kama yuko imara sana - na barakoa pia inamsumbua sana.
Ikiwa kuna timu ambayo inaweza kuisumbua Uhispania kuliko nyingine yoyote, ni Ufaransa.
Kwangu mimi, kwa matatizo ya Uhispania kwenye safu ya kiungo kutokana na kuumia Pedri itakuwa ni kesi ya nani atashinda vita katikati.
Uwezo wa safu ya kiungo ya Ufaransa ni kubwa na hapo ndipo mchezo utakapochezwa.
Huu utakuwa mchezo mkubwa kwa Antoine Griezmann, ukizingatia ametumia muda mwingi wa soka nchini Hispania kuliko Ufaransa, hivyo tunamhitaji yeye na Mbappe watafanya makubwa.
Nataka fainali ya Ufaransa-England na nadhani Ufaransa, kati ya washindi wanne wa nusu fainali, wana uzoefu mkubwa.
Wout Weghorst amekuwa silaha muhimu kwa Uholanzi |
Mwandishi wa mpira wa miguu wa Uholanzi, Jesper Langbroek:
Mchezo wa Uturuki nadhani ulionyesha Uholanzi wana mpango B - wakimtumia Wout Weghorst kama mshambuliaji huku Memphis Depay akiwa nyuma yake.
Jambo ambalo nimeona kwa timu hii ni kwamba wanahitaji kuamka ili wasonge mbele. Walifanya vyema dhidi ya Austria na kisha dhidi ya Romania walikuwa wazuri. Kisha wakaamka tena dhidi ya Uturuki.
Nadhani mshindi atatoka upande wa pili wa droo. Uingereza na Uholanzi bado hazijajaribiwa kweli; wamekutana na timu nzuri lakini hawajacheza na nchi kubwa.
Nadhani Uhispania itashinda kwa sababu wanacheza mpira mzuri kwa pamoja. England, Ufaransa na Uholanzi bado hawajatulizana, na muda unasonga.
No comments:
Post a Comment