Rick Dallaway ni mgonjwa aliyepandikizwa kinyesi nchini Uingereza.
"Wazo la upandikizaji wa kinyesi hakika ni la kushangaza," anakiri Rick Dallaway, akikumbuka wakati alipoalikwa kushiriki katika majaribio ya kliniki.
Mwanaume huyo mwenye umri wa miaka 50 amekamilisha mpango wa miezi miwili wa upandikizaji wa kila wiki wa kinyesi katika Chuo Kikuu cha Birmingham kwa matumaini ya kudhibiti dalili za ugonjwa sugu wa ini unaoitwa, sclerosing cholangitis (PSC).
"Sio tu kipande cha kinyesi," anacheka wakati anaelezea mchakato wa upandikizaji. "Kinatengenezwa, kinapitia mchakato katika maabara."
Kwa sasa hakuna tiba ya ugonjwa adimu wa Dallaway, isipokuwa upandikizaji wa ini kwa mgonjwa. Ugonjwa huu unaathiri kati ya watu sita na saba katika kila watu 100,000 nchini Uingereza na hupunguza umri wa kuishi kwa miaka 17 hadi 20.
Dallaway aligunduliwa kuwa na ugonjwa huo miaka minane iliyopita, alipokuwa na umri wa miaka 42.
"Nilikuwa na wasiwasi sana, na wasiwasi sana juu ya siku zijazo," anakumbuka. "
Ingawa Rick alikubali upandikizaji huu ili kutibu sclerosing cholangitis, nchini Uingereza inapendekezwa rasmi kwa wagonjwa walio na maambukizi makali ya Clostridium difficile (C. diff), ambao ni bakteria hatari wanaoweza kusababisha kuhara na mara nyingi huathiri watu ambao wamekuwa wakitumia dawa za maambukizi (antibiotics ) kwa muda mrefu.
Sampuli ya kiwango cha 50ml cha FMT kwa sasa inagharimu karibu dola za Marekani 1,700, kiwango ambacho wataalam wanasema ni chini ya gharama ya dawa za antibiotiki na matibabu ya hospitali. Kwa hali fulani, FMT inahitaji tu kusimamiwa mara moja.
Vituo vingine pia hutoa vidonge vya mdomo vilivyotengenezwa kutoka kwa bakteria wenye afya wanaopatikana kwenye kinyesi cha binadamu.
Unaweza pia kusoma:
Kwa kawaida watu wanaohitaji ini mpya, figo au moyo huweza kusubiri miezi au hata miaka kupata wafadhili wanaofaa.
Tofauti na viungo hivi vinavyohitajika sana, kinyesi cha binadamu kinapatikana sana na kwa urahisi , ingawa wazo la kupokea kinyesi cha mtu mwingine linaweza kuwafanya watu wengine wawe na wasiwasi.
Lakini Dallaway anaamini katika sayansi licha ya kwamba sio jambo la kawaida kwa wengi. Mke wake na marafiki zake wamekuwa wakiunga mkono juhudi zake.
"Hakuna aibu au wasiwasi," Dallaway anasema. "Kama kuna nafasi inaweza kufanya kazi, kwa nini isifanyike? Hayo ndio majibu niliyoyapata kutoka kwa marafiki na familia."
Katika mchakato wa upandikizaji wa kinyesi, kinyesi hukatwa katwa, kuchujwa, na kuvutwa kwenye sindano.
Kituo cha Tiba ya Microbiome cha Chuo Kikuu cha Birmingham (MTC) kilikuwa kituo cha kwanza kutoa huduma ya kwanza ya upandikizaji wa kinyesi (FMT) nchini Uingereza kwa kutoa sampuli za kinyesi kwa waganga kutibu mamia ya wagonjwa walio na maambukizi hayo na kufanya majaribio ya utafiti.
Katika kituo hicho, wafadhili hupitia mchakato mkali wa uchunguzi ambao unajumuisha historia ya kina ya matibabu, tathmini ya maisha, na upimaji wa vimelea katika damu na kinyesi chao.
Mara baada ya kuchambuliwa kabisa, sampuli za kinyesi zenye afya huhifadhiwa hadi miezi 12 katika jokovu lenye kipimo cha -80 ° C. Wakati mgonjwa anahitaji kupandikizwa kinyesi, kinyesi kilichohifadhiwa kilichochujwa hutiwa na kuvutwa kwenye sindano hadi ndani ya tumbo la mgonjwa.
"Ni vigumu katika nchi ambazo hazina akiba za kinyesi, lakini pendekezo litakuwa kutumia upandikizaji wa kinyesi (FM) kilichogandishwa ili kuruhusu muda wa kuwachunguza watu hawa vizuri," Profesa Tariq Iqbal, mkurugenzi wa Kituo cha Matibabu cha Microbiome, aliiambia BBC.
Wataalamu wanaonya kuwa 70% hadi 80% ya wagonjwa walio na hali sawa na Dallaway, PSC, pia wanaweza kupata ugonjwa wa vidonda vya utumbo (IBD), ambavyo vinaweza kusababisha maumivu makali ya tumbo na kuhara.
Dkt Palak Trivedi, mtaalamu wa magonjwa ya utumbo anayeongoza jaribio la matibabu anayofanyiwa Dallaway, anasema wanasayansi hawajui kwa nini matibabu hayo ya kinyesi yanasababisha ugonjwa wa vidonda vya tumbo IBD.
"Lengo letu ni kuhamisha vimelea wazuri wa utumbo kwenye utumbo wa wagonjwa walio na tatizo la CEP na kuona jinsi inavyoathiri ugonjwa wao wa ini," anaelezea profesa.
Kwa sasa, upandikizaji wa kinyesi sio chaguo la kwanza la matibabu linalotolewa kwa hali yoyote, anasema Horace Williams, mtaalamu wa tiba ya utumbo katika taasisi ya Imperial College London ambaye amesaidia kuendeleza miongozo rasmi juu ya upandikizaji huo.
Anasisitiza kuwa katika nchi kama Uingereza hutolewa tu kwa maambukizi makali ya Clostridium difficile (C. diff), sio hali nyingine, na anapendekeza kwamba wagonjwa ambao wanataka kupata matibabu kwa sababu nyingine wanapaswa kushiriki katika majaribio ya kliniki, kama alivyofanya Dallaway.
Wafadhili wanaotoa kinyesi hufanyiwa uchunguzi mkali, ikiwa ni pamoja na vipimo vya damu na kinyesi ili kugundua vimelea.
Benjamin Mullish, mtaalamu wa magonjwa ya utumbo (gastroenterologist ) katika taasisi ya Imperial College London na mwandishi mkuu wa miongozo ya British Society of Gastroenterology (BSG) kuhusu FMT, aliiambia BBC kwamba watu wengi hufanya upandikizaji wenyewe, ambao unaweza kuwa hatari sana.
Mtaalam wa matibabi ya kibaiolojia yanayohusisha vimelea Harriet Etheriedge, anasema kuwa bila wataalamu wenye uzoefu na miongozo wazi, tiba ya kinyesi-FMT inaweza kuwa na madhara, "hasa katika nchi maskini ambapo rasilimali za afya ni chache."
Matibabu hayo hata yamesababisha vifo katika hali nadra sana.
Mbali na Marekani na Ulaya, majaribio ya FMT yamefanyika katika nchi kama Brazil, Afrika Kusini na India.
Baadhi ya wagonjwa wamekuwa wakisita kukubali matibabu haya kutokana na kuchukizwa kwao na kinyesi, pamoja na imani mbalimbali za kitamaduni, kijamii na kidini kuhusiana na kinyesi.
"Watu wakati mwingine wanaweza kufikiri daktari anafanya mzaha," anasema Dk Piyush Ranjan, wa Taasisi ya tiba ya ini katika Hospitali ya Sir Ganga Ram nchini India.
Akizungumza kutokana na uzoefu wa kibinafsi, Ranjan anasema baadhi ya wagonjwa wako sawa zaidi kwa kukubali kinyesi kutoka kwa jamaa kuliko kutoka kwa mtu mwingine, hata kama amechunguzwa na ana afya nzuri.
Upandikizaji kwa kawaida hufanyika kwa vifaa vya colonoscopy, enema, au bomba maalum la nasogastric.
Uchunguzi mwingine wa watu zaidi ya 200 wenye maradhi hayo nchini Uingereza uligundua kuwa walipendelea zaidi kinyesi zaidi kutoka kwa chanzo kisichojulikana, kilichojaribiwa kuliko kutoka kwa mtu waliyemjua.
Katika utafiti huo huo, 37% ya washiriki awali walisema hawatakubali upandikizaji wa kinyesi, lakini baada ya kujifunza zaidi juu ya mchakato, takwimu hii iliongezeka hadi 54%.
"Elimu siku zote huvunja vikwazo vingi," Dkt Bret Palmer, ambaye aliongoza utafiti huo, aliiambia BBC.
Dallaway sasa ana matumaini kuwa majaribio yake yatafanikisha tiba ya ugonjwa wake adimu.
"Kama mtu angeniambia miaka 10 iliyopita kwamba kinyesi cha binadamu kinaweza kutibu magonjwa, nisingeamini kabisa," anasema. "Lakini sasa ni hali halisi na inaendelea."
No comments:
Post a Comment