Hadithi hii ya kuchekesha kuhusu simba mvivu iliyoandikwa kwenye karatasi, sasa ni kumbukumbu ya maisha ya mtoto aliyefariki wakati jengo la shule lilipoporomoka katika jiji la Jos nchini Nigeria.
Chidera Onovo, 15, alikuwa mvulana mtulivu ambaye alipenda kuchora na alikuwa kipenzi cha mama yake.
"Alihifadhi pesa zake za chakula cha mchana ili kununua biskuti ili kugawana na ndugu zake," Blessing Onovo anakumbuka. "Na yeye ndiye aliyegundua hisia zangu kila wakati na kuuliza: 'Mama uko sawa?'."
Ijumaa iliyopita asubuhi Chidera alienda shule ya upili na dadake mdogo Chisom lakini ni mmoja tu aliyerudi nyumbani.
Taarifa rasmi kutoka kwa serikali ya Nigeria zinasema wanafunzi 22 walifariki baada ya jengo la shule ya kibinafsi ya Saints Academy kuporomoka, katikati mwa jiji la Jos, lakini wakazi wa eneo hilo wanasema idadi hiyo inakaribia 50.
Wakitumia mikono na koleo, wazazi waliwatafuta sana manusura, na walifanikiwa kupenya na kuwaokoa baadhi ya watoto walionaswa kwenye vifusi. "Ilichukua takriban saa moja kabla tupate msaada," anasema babake Chidera, Chike Michael Onovo.
"Nilimuona binti yangu Chisom akitolewa nje. Nikafarijika, lakini niliendelea kupiga mayowe: 'Chidera mwanangu yuko wapi?'
Mwili wa mvulana huyo ulipatikana baadaye, ukiwa umepondwa na saruji iliyoanguka katika darasa lake kwenye ghorofa ya kwanza.
Victor Dennis mwenye umri wa miaka 43, pia alikuwa mmoja wa wazazi waliokuwa wakiwatatufuta sana watoto wao.
Hofu yake ilithibitishwa siku moja baadaye alipopata maiti ya mwanawe Emmanuel kwenye chumba cha kuhifadhi maiti cha eneo hilo.
"Mtoto wangu alikuwa mvulana mzuri," anaiambia BBC. "Hakustahili kufa. Walimuua mwanangu. Hakufanya chochote kibaya. Alienda shule kusoma tu."
Victor Dennis akishikilia picha ya mwanawe wa kiume, Emmanuel aliyefariki
Bwana Dennis anabubujikwa na machozi huku waombolezaji wakiimba wimbo wa kuaga katika mazishi ya mwanawe. Mama yake Emmanuel hakuwepo, ameshindwa kuhimili majonzi ya kumpoteza mwanawe akaamua kusalia nyumbani.
Watu wamekusanyika mjini Jos kusaidiana kwa hali na mali, na maisha ya watoto kadhaa yameokolewa kutokana na wafadhili wa damu ambao wametembelea hospitali za mitaa.
Subira yao ilivunjika baada ya jengo lingine kuporomoka nchini Nigeria. Wakazi wanadai watoto walihisi jengo likitikisika siku iliyotangulia.
"Nyenzo duni zilitumika -zingeweza kusababisha kuporomoka kwa jengo," anasema mdhibiti na msanifu mijengo Olusegun Godwin Olukoya, ambaye anaongoza Taasisi ya Wasanifu Majengo ya Nigeria katika jimbo la Plateau. "Uchunguzi wetu wa awali unaonyesha kuna uwezekano kanuni za ujenzi hazikungatiwa ."
Anaelekeza kidole xha lawama kwa wajenzi na mamlaka ya Nigeria, akiambia BBC:
“Kwa bahati mbaya, kutokana na aina ya jamii tunayoishi, ukosefu wa utashi umezuia mamlaka kupitisha mapendekezo yetu siku za nyuma.
"Watu wanataka kutumia njia ya mkato unapojaribu kuwapa ushauri wa kitaalamu kuhusu ujenzi, wengine wanahisi kuwa unataka kuwadhulumu au kuwakandamiza. Wanatumia watu wao katika nyadhifa za mamlaka kukwepa sheria."
Kufuatia kuporomoka kwa jengo la Saints Academy, gavana wa eneo hilo ameamuru ukaguzi wa kiufundi wa shule zote na majengo ya umma katika jimbo la Plateau, ambalo mji mkuu wake ni Jos.
Maafisa katika serikali yake wanasema haijabainika iwapo mmiliki wa shule hiyo, ambaye amefariki, aliwahi kuwa na kibali cha ujenzi wa eneo hilo.
BBC haikufanikiwa kupata maoni kutoka kwa wasimamizi wa shule hiyo.
Baadhi pia wanashuku kuwa shughuli za uchimbaji madini huenda ilichangia kuporomoka kwa jengo la shule hiyo, hivyo mkuu wa mkoa pia ameagiza kukamatwa kwa wachimbaji wadogo watakaokutwa wakichimba katika makazi ya watu jimboni humo.
Lakini maafisa wanashuku kuwa tatizo kuu lilikuwa jinsi shule hiyo ilivyojengwa.
"Hata kama mtu ambaye sio mtaalamu wa ujenzi, unaweza kubaini kwamba vifaa vinavyotumika katika ujenzi huo si vya kawaida.
Lakini tutachunguza chanzo cha ajali hiyo na kuwaadhibu watakaopatikana na hatia," Musa Ashom, Kamishna wa Habari wa Jimbo, anaiambia BBC.
Uchunguzi tofauti umeamriwa na wadhibiti na serikali
Ahadi kama hizo zilitoka kwa Waziri wa Makazi wa Nigeria, Ahmed Dangiwa, ambaye aliwakemea vikali watu "wasio waaminifu" ambao vitendo vyao alisema vimesababisha shule ya Jos kuporomoka na kusababisha hasara kubwa.
Lakini matamshi hayo yamechelewa kwa familia nyingi zilizofiwa, kama ile ya Chinecherem Joy Emeka.
Mtoto huyo mwenye umri wa miaka 13 alikuwa mmoja wa wacheza densi bora katika shule yake na alikuwa na ndoto ya kuwa daktari siku zijazo, anasema mamake Blessing Nwabuchi.
Chinecherem, au Chi Chi kama wapendwa wake walivyomuita, alikuwa akifanya mitihani yake ya mwisho wa mwaka siku aliyofariki.
Picha kama hii, kutoka kwa mahafali yake ya juu mwaka jana, ni ukumbusho vya thamani ya kile alichopata - na kila kitu ambacho huenda angelifikia maishani.
No comments:
Post a Comment