TBC YAPONGEZWA KWA KULINDA TASWIRA YA NCHI KIMATAIFA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Saturday, July 20, 2024

TBC YAPONGEZWA KWA KULINDA TASWIRA YA NCHI KIMATAIFA


Na Mwandishi Wetu, WHMTH, Dar es Salaam.


Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) limepongezwa kwa kuandaa vipindi vyenye maudhui yanayolinda maadili na taswira ya nchi kimataifa.

Pongezi hizo zimetolewa na Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Mhandisi Maryprisca Mahundi (Mb) tarehe 20 Julai, 2024 alipotembelea ofisi za Shirika hilo zilizopo barabara ya Nyerere na zile za Mikocheni jijini Dar es Salaam.


“Napenda kuwatia moyo kuwa hicho mnachokifanya ni cha kizalendo na kinawapa heshima hata kama kibiashara hamtapata matangazo ya kutosha lakini maudhui ya vipindi vyenu yanalinda maadili na taswira ya nchi”, amezungumza Mhandisi Mahundi.

Ameongeza kuwa, “Nitoe pongezi kwa Mkurugenzi Rioba umeweka alama ndani ya Shirika letu la TBC, nimekuwa nikikufuatilia sana na nimeona umetumika ipasavyo na kuwa mlezi wa watangazaji wengi”.

Akitoa salamu za Waziri, Mhe. Nape Moses Nnauye, amewataarifu kuwa masuala yao yote ya kisheria, maslahi ya watumishi na mapato ya Shirika yanaendelea kufanyiwa kazi kwa maelekezo ya Mhe. Rais Dkt. Samia.

Mkurugenzi Mkuu wa TBC, Dkt. Ayub Rioba amesema wao kama shirika dhima yao ni kuandaa vipindi vya elimu, historia, utamaduni na vinavyolinda maadili na tunu ya Taifa.

Amesisitiza kuwa, Shirika hilo linatoa taarifa za ukweli na uhakika kwa kutanguliza utaifa mbele kitu ambacho wakati mwingine kinawakosesha matangazo lakini wakiwa kama kiungo kati ya Serikali na wananchi wanaendelea kutekeleza majukumu yao ipasavyo.

No comments:

Post a Comment