Na WMJJWM, Iringa
Wakuu wa vyuo ya Maendeleo ya Jamii nchini wameagizwa kuhakikisha wanashirikisha jamii katika kubadili fikra ili kuwaletea wananchi maendeleo.
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima ametoa agizo hilo Julai 16, 2024 wakati akizungumza na wananchi wa kijiji cha Kitelewasi, kata ya Rungemba mkoani Iringa katika ziara yake kwenye chuo cha Maendeleo ya Jamii Rungemba.
"Ushirikiano wa chuo hiki na kijiji katika kubadilisha fikra kwa jamii umesababisha mwitikio wa wananchi walioweza kulima ekari 204 za parachichi zenye thamani karibia shilingi bilioni 4. Ni utajiri uliochochewa na chuo cha Maendeleo ya Jamii." amesema Waziri Gwajima.
Amepongeza jitihada zilizofanywa na chuo cha Rungemba za kuelimisha jamii kubadili fikra na kutaka vyuo vingine kuiga mfano huo.
Aidha, amevitaka vyuo hivyo kufanya midahalo shirikishi ya masuala ya mmomonyoko wa maadili, ukatili wa kijinsia na watoto, ndoa kufarakana, watoto kujilea wenyewe yanayotokana na mabadiliko makubwa ya kidijitali ili jamii zielewe na kuwa makini kuchagua mema na mabaya.
Kuhusu suala la uanagenzi, Waziri Gwajima amewaelekeza wakuu wa vyuo kuhakikisha wahitimu wapate taarifa ya fursa mbalimbali ziwawezeshe kujiajiri na kuendeleza ujuzi waliopata.
Mkuu wa Chuo hicho Kidubya Kulamiwa amebainisha kuwa chuo hicho kinaendelea na utekelezaji wa Programu za uendelezaji ujuzi na ushirikishwaji jamii kwa lengo la kutatua changamoto za kijamii ambapo wameanza na suala la lishe.
"Tulifanya utafiti katika kata 7 za mji wa Mafinga na kubaini kuna changamoto ya lishe na udumavu kwa asilimia 44. Kutokana na utafiti huo tumetoa elimu ya lishe kwa wananchi 2998 hadi sasa katika vijiji 7 kwenye kata 2" amesema Kulamiwa.
Amebainisha kwamba moja ya miradi ya uzalishaji mali ikiwa ni sehemu ya mafunzo ni shamba la parachichi lenye ekari 25 kwa sasa, miti 1500 na wameshavuna matunda ya thamani ya mil.5.1. pamoja na Shamba la nyuki lenye mizinga 21 kwa sasa.
Katika ziara hiyo, Waziri Dkt. Gwajima ametembelea Mradi wa Ujenzi wa ukumbi wa Mihadhara utakaogharimu jumla ya sh. milioni 300 hadi kukamilika kwake na unaotarajiwa kuchukua wanafunzi 600, ujenzi wa Maabara ya kompyuta, amezindua shamba la parachichi la chuo na kukabidhi vikapu 100 kwa wanakijiji wa Kitelewasi kwa ajili ya shughuli za uvunaji.
No comments:
Post a Comment