SERIKALI KUWEKA MIFUMO THABITI UTEKELEZAJI SERA YA WAZEE. - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Friday, January 16, 2026

SERIKALI KUWEKA MIFUMO THABITI UTEKELEZAJI SERA YA WAZEE.



Na Said Said WMJJWM - Dodoma


Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima, amesema kuanzishwa kwa sekretarieti ya utekelezaji wa Sera ya Wazee ya Mwaka 2003 Toleo la Mwaka 2024 ni hatua muhimu ya Serikali katika kuweka mifumo thabiti ya uratibu, ufuatiliaji na tathmini ya utekelezaji wa Sera ya hiyo katika ngazi zote za utawala.

Akizungumza na Sekretarieti ya Uratibu wa Utekelezaji wa Sera hiyo kwa njia ya mtandao kidijitali tarehe 16 Januari, 2026, jijini Dodoma amesisitiza kuwa sekretarieti itakuwa kiungo muhimu kati ya Wizara za Kisekta, Taasisi za Umma, Mamlaka za Serikali za Mitaa na wadau wa maendeleo katika kuhakikisha huduma zinazowalenga wazee zinapangwa na kutekelezwa kwa ufanisi na kwa kuzingatia mahitaji halisi ya walengwa.

Aidha, ametoa wito kwa Wizara za Kisekta, Mikoa na Halmashauri kuhakikisha masuala ya wazee yanaingizwa kikamilifu katika mipango na bajeti zao za kila mwaka, pamoja na kuwasilisha taarifa za utekelezaji kwa wakati huku akisisitiza kuwa mafanikio ya Sera ya Wazee yatategemea dhamira ya pamoja ya Serikali na wadau wote katika kuwajali, kuwathamini na kuwalinda wazee kama hazina ya Taifa.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhandisi Maryprisca Mahundi, amewataka waratibu wa masuala ya wazee kuhakikisha wanasimamia kikamilifu utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Wazee kwa vitendo badala ya kubaki kwenye maandiko pekee.

“Ni dhahiri kuwa tunalo jukumu la pamoja la kuhakikisha Sera ya Taifa ya Wazee inatekelezwa kwa vitendo na kwa ufanisi katika Wizara za kisekta na taasisi zetu. Ushirikiano, uwajibikaji na uratibu wa karibu ndiyo msingi wa kufanikisha dhamira hii” amesema Mhe. Maryprisca

Kikao hicho kimejumuisha wadau kutoa katika Wizara za Kisekta, Mikoa, Wilaya na Majukwaa mbalimbali pamoja na mambo mengine imezinduliwa Sekretarieti ya Kitaifa ya utekelezaji wa Sera hiyo.




No comments:

Post a Comment