
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano, Mhe.Deus Sangu,akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma Januari 16, 2026.
Na Okuly Julius , OKULY BLOG, Dodoma
Jumla ya vijana 5,746 wamechaguliwa kujiunga na Mafunzo ya Uanagenzi kwa mwaka 2025/2026, kati ya vijana 20,247 walioomba kushiriki mafunzo hayo yaliyotangazwa na Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma Januari 16, 2026, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano, Mheshimiwa Deus Sangu, amesema vijana hao wataanza mafunzo yao rasmi tarehe 19 Januari, 2026 katika vyuo mbalimbali vya ufundi stadi walivyopangiwa nchini.
Amesema majina ya vijana waliochaguliwa pamoja na vyuo walivyopangiwa yatatangazwa kuanzia Januari 17, 2026 kupitia tovuti ya Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano, vyombo vya habari pamoja na mbao za matangazo katika vyuo husika.
Mheshimiwa Sangu amebainisha kuwa mafunzo hayo ni sehemu ya utekelezaji wa Programu ya Taifa ya Kukuza Ujuzi kwa njia ya Uanagenzi, inayolenga kuwawezesha vijana kupata ujuzi unaoendana na mahitaji ya soko la ajira ili kuongeza fursa za kuajiriwa au kujiajiri.
Ameeleza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, imeendelea kuweka mkakati wa makusudi wa kuimarisha rasilimali watu kupitia mafunzo ya vitendo yatakayoongeza ushindani wa nguvukazi ya taifa katika soko la ajira la ndani na nje ya nchi.
Kwa mujibu wa Waziri huyo, mafunzo hayo yanatekelezwa kwa ushirikiano kati ya Serikali na wadau wa UTATU PLUS, wakiwemo vyama vya waajiri, vyama vya wafanyakazi, sekta binafsi na wadau wengine wa maendeleo, na yanajumuisha mafunzo ya uanagenzi, mafunzo ya uzoefu kwa wahitimu, kukuza ujuzi kwa wafanyakazi pamoja na urasimishaji wa ujuzi uliopatikana nje ya mfumo rasmi wa elimu.
Ameongeza kuwa Serikali itagharamia ada ya mafunzo hayo kwa asilimia 100, huku wazazi au walezi wakitakiwa kugharamia nauli ya kwenda chuoni na kurudi nyumbani kwa kuwa mafunzo hayo ni ya kutwa.
Katika hatua nyingine, Waziri Sangu ametoa wito kwa vijana waliochaguliwa kuripoti vyuoni kwa wakati, kuwa na nidhamu na kuzingatia sheria na taratibu za vyuo, huku akiwataka wazazi na walezi kutoa ushirikiano wa karibu ili kuhakikisha vijana wanahitimu mafunzo hayo kwa mafanikio.
Aidha, amezitaka taasisi na vyuo vilivyochaguliwa kutoa mafunzo hayo kuhakikisha vinatoa elimu bora, usimamizi wa karibu na mazingira rafiki ya kujifunzia ili vijana waweze kupata ujuzi stahiki unaohitajika katika soko la ajira.
Serikali imeeleza kuwa utekelezaji wa programu hiyo ni hatua muhimu katika kukuza ajira, kupunguza tatizo la ukosefu wa ajira miongoni mwa vijana na kuchochea maendeleo ya kiuchumi kupitia uzalishaji na ubunifu wa vijana wenye ujuzi.

No comments:
Post a Comment