KAMATI YA MIUNDOMBINU YASHAURI UJENZI WA MADARAJA MAENEO YENYE USAFIRI WA VIVUKO. - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Tuesday, August 20, 2024

KAMATI YA MIUNDOMBINU YASHAURI UJENZI WA MADARAJA MAENEO YENYE USAFIRI WA VIVUKO.


Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu imeishauri Wizara ya Ujenzi kufanya usanifu kwenye maeneo yote yenye huduma za usafiri wa Vivuko na kupanga mikakati ya kudumu ya kujenga madaraja katika baadhi ya maeneo ili kupunguza changamoto zinazokabili uendeshaji wa huduma hizo.

Ushauri huo umetolewa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Selemani Kakoso(Mb) leo Agosti 20, 2024 jijini Dodoma wakati Kamati ikipokea taarifa ya ukarabati na ujenzi wa vivuko vipya kutoka kwa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA)

Kamati imeishauri TEMESA kufanya tafiti za kina na kuweka mikakati ya miaka mitano hadi kumi ya kuboresha utoaji huduma za vivuko ikiwemo gharama za uendeshaji, mahitaji halisi ya vivuko pamoja na maksio halisi ya wananchi wanaohitaji huduma za vivuko nchini.

Kadhalika, Kamati imeshauri Wizara ya Ujenzi kuwa na mkakati wa ubunifu wa kusaidia kupunguza msongamano wa magari barabarani kwa kuanzisha mradi wa utoaji wa huduma za vivuko/meli katika maeneo ya Kigamboni - Mbweni - Bagamoyo.

Kamati imeiagiza Wizara ya Ujenzi kusimamia TEMESA iweze kukusanya madeni wanayodai kwa Taasisi za Serikali ili kuisaidia Wakala huo kujiendesha pamoja kutoa gawio kwa Serikali.


Akiwasilisha taarifa, Waziri wa Ujenzi Innocent Bashungwa ameeleza kuwa katika mwaka wa fedha 2024/25, TEMESA imetenga kiasi cha Bilioni 27 kwa ajili ya kugharamia miradi saba ya ujenzi wa vivuko vipya, miradi sita ya ukarabati wa vivuko pamoja na kuanza ukarabati wa vivuko saba ikiwemo Mv Kigamboni, Mv Mwanza, Mv Ukara II, Mv Pangani II, Mv Malagarasi, Mv Sabasaba na Mv Mafanikio.

Bashungwa ameongeza kuwa Wizara kupitia TEMESA ipo katika hatua za mwisho za kusaini mkataba wa pamoja (Joint Venture) na kampuni ya Azam Marine ili kurahisisha huduma za usafiri katika kivuko cha Kigamboni ambapo amesisitiza ubia huo unarajiwa kuanza mwezi Oktoba mwaka huu.


Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa TEMESA, Lazaro Kilahala ameeleza kuwa TEMESA inaendesha vivuko 32 katika vituo 22 Tanzania Bara ambapo hadi kufikia mwezi Agosti, 2024 jumla ya vivuko 21 vinaendelea kutoa huduma katika vituo 16 huku vivuko 11 vipo kwenye ukarabati na matengenezo.

No comments:

Post a Comment