MBUNGE wa Singida Mashariki Miraji Mtaturu ametembelea na kugua ujenzi wa miradi ya maji katika Kijiji Cha Mang'onyi ,mradi wa maji wa Kijiji cha Sakaa na Ujenzi wa Tanki la Maji katika Kijiji Cha Minyinga ambayo kukamilika kwake kutaondoa adha ya wananchi kutembea umbali mrefu kusaka maji.
Akiwa katika Kijiji Cha Mang'onyi ambapo mradi umepewa jina la kisima cha Mama Samia,Mtaturu amesema kwenye Bajeti ya Mwaka 2023/2024,mradi huo ulitengewa Sh Milioni 390 kupitia fedha za Mfuko wa Maji ambapo hadi kufikia Juni 30,2024, serikali imetoa kiasi cha Sh Milioni 150 tu.
"Awamu hii ya utekelezaji itahusisha ujenzi wa nyumba ya mashine,Tenki la kuhifadhia Maji lita 50,000 juu ya mnara wa mita 6, ujenzi wa miundombinu ya bomba Kilometa 5.1, ujenzi wa vituo 4 vya kuchota maji pamoja na ufungaji wa mfumo wa kusukuma maji,".amesema.
Aidha amesema Mradi huo unalenga kuingiza maji majumbani kutokana na hali halisi ya mazingira ya Mang'onyi ambayo yanaakisi mazingira ya mjini na kwamba Miundombinu ya bomba imesanifiwa kuweza kuingiza huduma ya maji majumbani na hivyo kuwapunguzia wananchi umbali wa kutembea.
Mtaturu amesema bomba zimepitishwa karibu na makazi ya wananchi ili iwe rahisi kuunganisha maji ambapo kukamilika kwa mradi huo pia kutasaidia kuondoa changamoto ya maji safi na salama kijiji cha Mang'onyi na baadhi ya vitongoji ya vijiji vya Tupendane na Mwau vilivyopo kata ya Mang'onyi.
Aidha Mbunge Mtaturu ametembelea mradi wa maji wa Kijiji Cha Sakaa uliopo Kata ya Misughaa ambao utekelezaji wake umefikia asilimia 90.
Mradi huo umetengewa kiasi Cha Sh Milioni 323.5 ambapo kazi zilizobakia ni kupaka rangi kwenye tenki.
Pia katika mradi wa ujenzi wa Tenki Kijiji Cha Minyinga uliotengewa Sh Milioni 269.5 utekelezaji wake umefikia asilimia 80 ambapo Tenki limeshafunikwa na mnara umeshapigwa plasta.
No comments:
Post a Comment