KASEKENYA AWATAKA WAKANDARASI KUTUMIA VEMA FURSA ZA BENKI - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Tuesday, August 6, 2024

KASEKENYA AWATAKA WAKANDARASI KUTUMIA VEMA FURSA ZA BENKI


NAIBU Waziri wa Ujenzi Eng. Godfrey Kasekenya amewataka Wakandarasi nchini kutumia vizuri fursa za kibenki kukuza mitaji na hivyo kumudu kupata miradi mikubwa ya ujenzi ili kukuza uchumi binafsi na taifa kwa ujumla.

Naibu Waziri wa Ujenzi, Eng. Kasekenya ameyasema hayo leo jijini Dar es Salaam alipokuwa akizinduwa Maboresho ya Huduma za Kibenki kwa Makandarasi Wazawa, kwa Benki ya NMB ambapo imeongeza Kiwango cha Dhamana za Kuombea Kazi kutoka Sh. Bilioni 2.5 hadi Sh. Bilioni 5, kiwango cha Dhamana za Miradi kutoka Sh. Bilioni 1.5 hadi Sh. Bilioni 3.


Akifafanua zaidi, Naibu Waziri Kasekenya amesema fursa hizo zinaendana na mikakati ya Serikali ya kukuza uchumi wa wakandarasi wazawa na hivyo kusababisha fedha nyingi za miradi ya ujenzi kubaki nchini badala ya kwenda nje ya nchi.

"Uaminifu, weledi na uzalendo kwa wakandarasi kutawezesha benki nyingi kutoa mikopo na fursa nyingi na kukuza sekta ya wakandarasi", amesisitiza Eng. Kasekenya.

Aidha ameipongeza Benki ya NMB kwa mikakati yake ya kuwawezesha Wakandarasi hususan wazawa hali itakayokuza sekta ya ujenzi nchini.

"Serikali inatarajia fursa hizi na nyingine zitakazotolewa zitawawezesha wakandarasi wazawa kushindana na wakandarasi wa nje na kupata miradi mikubwa ya ujenzi na hivyo kuongeza ujuzi katika ujenzi wa miradi na kutoa fursa nyingi za ajira", amesisitiza.

IMETOLEWA NA KITENGO CHA HABARI NA MAWASILIANO


No comments:

Post a Comment