Naibu Waziri, Ofisi ya Rais UTUMISHI na Utawala Bora Mhe. Deus Sangu amewataka viongozi wa Idara ya Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu, Idara ya Uendelezaji wa Sera na Idara ya Uendelezaji Taasisi kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi ili kurahisisha utendaji kazi wa watumishi wa umma kwenye Wizara na Taasisi mbalimbali za umma.
Amesema hayo leo tarehe 12 Agosti, 2024 wakati Idara hizo zilipokuwa zikimpitisha kwenye majukumu yao kwa nyakati tofauti ikiwa ni sehemu ya ratiba yake ya kujifunza namna Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma inavyofanya kazi.
Mhe. Sangu amesema watumishi wa ofisi yake wanatakiwa kupewa mafunzo ya mara kwa mara ili waweze kwenda na wakati na wawe na uwezo mkubwa wa kuwahudumia watumishi wengine.
“Ninaamini bajeti inaweza kuwa kikwazo lakini, ninaelekeza itafutwe namna bora ambayo inaweza kutumia bajeti ndogo na watumishi wengi wakapata mafunzo”.
Aidha, ameelekeza idara ya Uendelezaji Taasisi kupitia miundo ya taasisi, kufuatilia na kutoa onyo kali kwa taasisi ambazo zimepewa miundo mipya lakini zinaendelea kutumia ya zamani kwa maslahi binafsi, hivyo kuongeza gharama za uendeshaji wa Serikali.
Hali kadhalika, ametoa rai kwa Idara ya Uendelezaji Sera kupitia na kuhuisha Kanuni za Kudumu za Utumishi wa Umma za Mwaka 2009 kwa kuwa watumishi walio wengi wanalalamikia uwepo wa vipengele ambavyo vimepitwa na wakati.
Mhe. Sangu anaendelea na ratiba ya kujifunza majukumu ya idara mbalimbali katika ofisi yake kwa muda wa siku nne (4) mfululizo kuanzia tarehe 12 hadi 15 Agosti, 2024 katika ukumbi mdogo wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mtumba Jijini Dodoma.
No comments:
Post a Comment