MPANGO WA SHULE SALAMA KWA MAENDELEO YA WANAFUNZI. - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Wednesday, August 14, 2024

MPANGO WA SHULE SALAMA KWA MAENDELEO YA WANAFUNZI.


Afisa Elimu wa Mkoa wa Singida, Dkt. Elipidus Baganda, amesema Serikali imeanzisha Mpango wa Shule Salama katika shule za sekondari nchini kwa lengo la kuboresha mazingira ya ufundishaji na ujifunzaji, pamoja na kuongeza ulinzi na usalama wa watoto.

Ameyasema hayo wakati akizungumza na washiriki wa mafunzo maalum ya Mpango wa Shule Salama, yaliyowakutanisha washiriki 275 kutoka mikoa ya Singida, Shinyanga, Tabora, na Simiyu. Kwa siku tatu yamefanyika mkoani Singida, yakilenga kuwajengea uwezo washiriki ili kuhakikisha shule za sekondari zinatoa elimu bora kwa kuondoa vikwazo mbalimbali vinavyowakabili wanafunzi.

Mafunzo haya yamehusisha wenyeviti wa bodi za shule za sekondari 150, maafisa 12 kutoka ngazi za mikoa, maafisa maendeleo ya jamii ngazi ya mkoa, pamoja na waratibu wa Mpango wa Shule Salama. Aidha, waratibu wa programu ya SEQUIP pia walishiriki katika mafunzo haya, ambayo ni sehemu ya Mpango wa Kuboresha Elimu ya Sekondari wa miaka mitano (2020-2025).

Dkt. Baganda alibainisha kuwa kumekuwepo na changamoto ya mdondoko wa wanafunzi katika shule za msingi na sekondari, jambo linalozuia wanafunzi kufikia malengo ya kielimu ambapo amesema Serikali imechukua hatua mbalimbali kupambana na changamoto hiyo ikiwa ni pamoja na kutoa elimu bila malipo na kujenga shule za sekondari karibu na makazi ya jamii, ili kupunguza umbali wa kufuata shule.

"Lengo kuu la mafunzo haya ni kuwapatia stadi na mbinu za usimamizi bora wa shule za sekondari ili kuhakikisha elimu inayotolewa inakidhi viwango vilivyokusudiwa. Mafunzo haya yanazingatia kuondoa vikwazo kama vile ukosefu wa chakula, utoro, na matumizi ya viboko, ambavyo mara nyingi huzuia wanafunzi kufikia malengo yao ya ufaulu"amesema Dkt.Bganda

Pia, Dkt. Baganda amewashukuru wadau wote wanaoshiriki katika kusimamia utekelezaji wa mpango huo na kuwataka washiriki wa mafunzo haya kujadiliana na kubadilishana uzoefu ili kuboresha utekelezaji wa mpango wa Shule Salama na kuwataka washiriki kutumia mafunzo hayo kuibua mbinu mpya za kuboresha mazingira ya shule.



No comments:

Post a Comment