

Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro imeahidi kuanza kutenga bajeti sambamba na kuwashirikisha katika vikao, mikutano na shughuli nyinginezo Waratibu wa Mfumo wa Anwani za Makazi (NaPA) ngazi ya Wilaya ili kusaidia sekta zote kuona umuhimu wake.
Ahadi hiyo imetolewa na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro mkoani Arusha, Bw. Thomas Nade wakati akijibu hoja zilizowasilishwa na Waratibu wa Anwani za Makazi Taifa na Wilaya waliofika ofisini kwake tarehe 26 Agosti, 2024 kutoa mrejesho wa zoezi la Uhakiki wa Taarifa za Anwani za Makazi wilayani humo.
Bw. Nade ambaye pia ni Afisa Maendeleo ya Jamii na Mratibu wa TASAF Wilaya ya Ngorongoro, amesema kutokana na umuhimu wa elimu, miundombinu na mfumo wenyewe wa Anwani za Makazi, atahakikisha analifikisha kwenye vikao vya maamuzi ili katika robo ya pili ya mwaka wa fedha itengewe kiasi fulani.


Awali waratibu hao walitembelea Ofisi ya Mtendaji Kata ya Engurosambu Kijiji cha Engurosambu kukagua maendeleo ya Uhakiki ambapo changamoto iliyoainishwa na watendaji hao wa Kata, Kijiji na Mtaa ni upatikanaji wa mtandao na umbali wa boma moja hadi nyingine inayochangiwa na jiografia ya eneo hilo.
Naye Bw. Jasson Kalile, Mtaalamu wa Mfumo wa Anwani za Makazi kutoka wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari na ambaye anasimamia Kata mbili ikiwemo ya Engurosambu katika zoezi hilo, amesema hadi kufikia tarehe 26 Agosti zaidi ya asilimia 70 ya Anwani zilikuwa zimesasishwa.





Kata hiyo ni miongoni mwa Kata mbili za Ngorongoro zilizo mpakani mwa Kenya na Tanzania zenye changamoto ya eneo kubwa na mwingiliano wa wananchi wa nchi jirani ya Kenya pamoja na mawasiliano duni ya mtandao wa simu na intaneti.
No comments:
Post a Comment