Naibu Waziri Ofisi ya Rais - TAMISEMI Mhe. Zainab Katimba amemwelekeza mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Muleba mkoa wa Kagera akamilishe haraka hatua za manunuzi na kupata mkandarasi wa ujenzi wa soko la kisasa la Muleba na ahakikishe ujenzi unakamilika kwa muda wa miezi sita.
Maelekezo hayo ya Mhe. Katimba ameyatoa kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais - TAMISEMI Mhe. Mohamed Mchengerwa kwenye mkutano wa hadhara wa Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi - CCM Mhe. Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi uliofanyika Agosti 11,2024 Muleba Mjini wakati akijibu kero za wananchi na kueleza mafanikio ya serikali ya awamu ya sita chini ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan,Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
“Ujenzi wa soko hilo upo katika hatua ya manunuzi na kupata mkandarasi na akipatikana mkandarasi inabidi ajenge ili wananchi waanze kutumia soko hili kwa maana lilikuwepo lakini linaboreshwa na kwa hatua hii naomba kumsisitiza mkurugenzi aweze kuharakisha taratibu za manunuzi na mkandarasi apatikane na ndani ya miezi sita ajenge soko hilo ili wananchi waanze kulitumia kwasababu fedha ipo bilioni mbili” Amesema
Mhe. Katimba ameendelea kumsisitiza mkurugenzi wa Halmashauri ya Muleba kuwa soko hilo litakapokamilika na kuanza kutoa nafasi kwa wafanyabiashara lizingatie nafasi za wafanyabiashara waliopisha eneo hilo kwaajili ya ujenzi ili waendelee na shughuli zao.
Aidha, Mhe. Katimba amewaeleza wananchi wa Wilaya ya Muleba kuwa katika kipindi cha miaka mitatu ya serikali ya awamu ya sita kumekuwa na ongezeko la bajeti katika sekta ya barabara kupitia TARURA kutoka Bil.1.3 hadi Bil. 4.3 kwa mwaka ambayo ni ongezeko la zaidi ya asilimia 230 ya bajeti kwa mwaka.
Mhe. Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi amehitimisha ziara yake katika mkoa wa Kagera kwa mkutano wa hadhara katika wilaya ya Muleba akielekea mkoa wa Geita akiwa ameambatana na viongozi mbalimbali wa Chama na Serikali akiwepo Mhe. Zainab Katimba ,Naibu Waziri Ofisi ya Rais- TAMISEMI.
No comments:
Post a Comment