DKT. MFAUME: UDHIBITI WA TAKA NGUMU UWE KAZI YA KUDUMU, SI YA WAKATI WA DHARURA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Friday, September 25, 2026

DKT. MFAUME: UDHIBITI WA TAKA NGUMU UWE KAZI YA KUDUMU, SI YA WAKATI WA DHARURA


Na OWM–TAMISEMI, Dodoma


Mkurugenzi wa Idara ya Afya, Lishe na Ustawi wa Jamii Ofisi ya Waziri Mkuu – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM–TAMISEMI), Dkt. Rashid Mfaume, amekitaka Kikosi Kazi cha Taifa cha Uratibu wa Utekelezaji wa Afua za Udhibiti wa Taka Ngumu na Usafi wa Miji kufanya kazi kwa mwendelezo badala ya kusubiri tahadhari za mafuriko au milipuko ya magonjwa.

Dkt. Mfaume ametoa wito huo leo, Septemba 25, 2026, jijini Dodoma, wakati akifungua kikao cha kwanza cha kikosi kazi hicho. Amesema vikao vya kitaalamu na ushauri wa mara kwa mara vitasaidia kukabili changamoto za taka kabla hazijaleta madhara kwa afya ya wananchi na mazingira.

Amesema kikosi kazi kinapaswa kuweka vipaumbele vya pamoja, kuratibu afua zinazoendelea na kutoa ushauri kuhusu matumizi bora ya rasilimali. Vipaumbele hivyo ni pamoja na ujenzi wa madampo ya kisasa, upatikanaji wa magari na vifaa vya kukusanyia taka, na uwekezaji katika teknolojia za urejelezaji.

“Tunataka mwisho wa siku watu wengine waje kujifunza kwetu,” amesema Dkt. Mfaume, akisisitiza umuhimu wa kuwa na Miji na Halmashauri safi, zinazokinga wananchi dhidi ya magonjwa na madhara yanayohusiana na uchafuzi wa mazingira.

Naye Mratibu wa Huduma za Afya na Usafi wa Mazingira wa OWM–TAMISEMI, Bw. Selemani Yondu, amesema taarifa ya mwaka 2025/2026 inaonesha kuwa Halmashauri 184 nchini huzalisha wastani wa tani 666,604 za taka ngumu kwa mwezi, lakini asilimia 55.3 tu hukusanywa. Takriban tani 300,000 hubaki bila kukusanywa kila mwezi; asilimia 15 tu ya Halmashauri zina madampo ya kisasa, huku Halmashauri 22 zikiwa hazina maeneo rasmi ya kutupa taka.

Bw. Yondu amesema uzoefu wa Halmashauri za Ilemela, Msalala, Jiji la Mbeya na Mji wa Bariadi unaonesha kuwa matokeo yanaweza kuboreshwa kwa kutumia bajeti za ndani, kuwekeza katika miundombinu na kuimarisha uongozi. Amesisitiza pia ushirikishwaji wa jamii, sekta binafsi na wakusanyaji taka wasio rasmi katika utenganishaji na urejelezaji wa taka.

Kikao hicho kimewakutanisha wawakilishi wa wizara na taasisi za Serikali, Sekretarieti za Mikoa, Mamlaka za Serikali za Mitaa, Wadau wa Maendeleo, asasi za kiraia na sekta binafsi ili kuimarisha ushirikiano katika udhibiti wa taka ngumu na usafi wa miji nchini.

No comments:

Post a Comment