
NEW YORK, Marekani.
Rais wa Namibia Mhe. Netumbo Nandi-Ndeitwah amesema dhamira ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kulinda afya na utu wa wanawake na watoto inagusa moja kwa moja mustakabali wa Afrika, akisisitiza kuwa uwekezaji katika afya ya mama na mtoto si matumizi ya kawaida bali ni uwekezaji katika watu, uchumi na maendeleo endelevu.
Rais Netumbo amesema hayo wakati wa mkutano wa Mkutano wa Ngazi ya Juu wenye ajenda isemayo “Uhamasishaji kwa Ajili ya Enzi Mpya: Wanawake Wanaoongoza katika Afya ya Mama na Mtoto kwa Wote” (Advocacy for a New Era: Women Leading Maternal and Child Health for All, “SHE RISES) ulioandaliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt.Samia Suluhu Hassan ambaye ni kinara wa Umoja wa Afrika katika afya ya Mama na Mtoto, pembezoni mwa Mkutano wa 81 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA 81), New York nchini Marekani.
Ametoa wito kwa Mataifa ya Afrika kuongeza uwezo wa ndani wa kugharamia huduma hizo badala ya kutegemea misaada ya nje pekee, akisisitiza kuwa maendeleo ya Bara la Afrika hayawezi kutenganishwa na afya ya watu wake.
Namibia imeahidi kuendelea kushirikiana na Tanzania katika utekelezaji wa jukumu hilo la Umoja wa Afrika.
Akiwasilisha uzoefu wa Tanzania, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Deogratius Ndejembi amesema uwekezaji huo tayari umeanza kupata mafanikio, ambapo kati ya mwaka 2015 na 2022 vifo vya uzazi vilipungua kutoka 556 hadi 104 kwa kila vizazi hai 100,000, huku vifo vya watoto walio chini ya miaka mitano vikishuka kutoka 67 hadi 43 kwa kila vizazi hai 1,000. Bajeti ya afya imeongezeka kutoka takribani Sh bilioni 780 mwaka 2015 hadi Sh trilioni 1.8 mwaka wa fedha 2026/27, wakati mfumo wa M-Mama ukiwa umewezesha zaidi ya rufaa 150,000 za dharura kwa akina mama na watoto wachanga hadi Agosti 2026. Hatua hizo, amesema, zinaonesha kuwa utashi wa kisiasa unapounganishwa na rasilimali na utekelezaji, unaweza kuleta mabadiliko yanayogusa maisha moja kwa moja.
Katika ngazi ya bara, Mhe. Ndejembi amesema Rais Samia, akiwa Kinara wa Umoja wa Afrika katika Afya ya Mama na Mtoto, anatumia nafasi hiyo kusukuma Mpango wa Umoja wa Afrika wa Mama, Mtoto mchanga, Mtoto na afya ya vijana balehe (African Union Champion Roadmap for Maternal, Newborn, Child and Adolescent Health), ikiwemo ajenda ya “sifuri tatu” ambayo inalenga kutokuwepo kwa kujifungulia nyumbani, kutokuwepo kwa vifo vya mama na watoto wachanga vinavyoweza kuzuilika, na kutokuwepo kwa watoto ambao hawajapata chanjo.
Kupitia ya ajenda ya “SHE RISES”, Tanzania pia inataka wanawake wasibaki kuwa wapokeaji wa huduma pekee, bali wawe sehemu ya uongozi na maamuzi yanayoamua mwelekeo wa mifumo ya afya.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Idadi ya Watu na Afya ya Uzazi (UNFPA), Bi. Diene Keita, amepongeza uongozi wa Rais Samia na nafasi ya Tanzania katika kuifanya afya ya mama na mtoto kuwa ajenda ya kisiasa ya Afrika. Amesisitiza kuwa mafanikio yanahitaji utashi wa kisiasa unaoonekana kwenye bajeti, uwekezaji katika huduma za uzazi na kuimarishwa kwa wakunga kama nguzo muhimu ya kuokoa maisha. UNFPA imeahidi kuendelea kuunga mkono juhudi hizo, ikisisitiza umuhimu wa viongozi na nchi vinara zinazoweza kugeuza dhamira za kimataifa kuwa huduma na matokeo halisi kwa wanawake na watoto.
Mkurugenzi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) kanda ya Afrika Dkt. Mohamed Janabi amesema dhamira ya kisiasa ikiendana na uwekezaji, uwajibikaji na vitendo, maisha ya mama na mtoto yataendelea kuokolewa. Amempongeza Rais Dkt. Samia kwa uongozi wake katika afya ya mama na mtoto kwa kuwa suala hilo ni la kimaendeleo, kiuchumi na haki.
Amesema Wanawake ndio nguzo katika mifumo ya afya kwa kuwa wanachangia kiasi kikubwa katika utoaji wa huduma za afya ikiwa asilimia 70 ya watendaji katika sekta ya afya barani Afrika ni wanawake. Dkt. Janabi amesema licha ya hayo bado idadi ya wanawake katika utoaji wa maamuzi imebaki asilimia 25 pekee.
Amesema ajenda ya “SHE RISES” ni kuhakikisha wanawake wanashiriki katika kutunga sera, kupanga bajeti, vipaumbele na uongozi utakaotoa matokeo bora kwa afya ya mama na mtoto.
Awali akitoa maelezo kuhusu Mkutano huo, Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Umoja wa Mataifa New York, Mhe. Togolani Mavura amesema mkutano huo unapaswa kuwa chachu ya wajibu kwaajili ya kuhakikisha ajenda ya afya ya mama na mtoto inapewa kipaumbele na huduma kuwa bora na sawa katika maeneo mbalimbali duniani.
Kwa Tanzania, SHE RISES inabeba hoja pana zaidi ya afya: kwamba kuokoa maisha ya mama na mtoto kunahitaji uongozi, fedha na uwajibikaji, lakini pia sauti ya mwanamke katika meza ambako maamuzi hayo yanafanyika. Ndiyo msingi wa ujumbe unaosukumwa kutoka New York kwenda Afrika na duniani mwanamke anapoinuka, Mama anaishi; Mama anapoishi, Mtoto anastawi; na Mtoto anapostawi, Taifa linainuka.
Mkutano huo, umehudhuriwa na Viongozi mbalimbali wa ndani na nje ya Bara la Afrika, Viongozi wakuu wastaafu akiwemo Rais wa Awamu ya Nne wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Jakaya Kikwete, Wakuu wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa, wadau wa sekta ya afya duniani pamoja na watunga sera.










No comments:
Post a Comment