Na Mwandishi Wetu Dar es Salaam
Wakala wa Vipimo Mkoa wa Dar es Salaam imeendesha zoezi la ukaguzi wa kushtukiza katika maduka mbalimbali ya kuuzia nondo ili kujiridhisha kama bidhaa hizo zipo katika Vipimo sahihi vinavyokubalika kisheria ikiwa ni katika upande wa kuhakiki urefu wa nondo, upana pamoja na alama zinazopaswa kuandikwa kwenye nondo.
Akizungumza wakati wa zoezi hilo, Afisa Vipimo Mwandamizi Bw. Abdul Kassim ameeleza kuwa kwa mujibu wa Sheria ya Vipimo Sura Na. 340 ukaguzi wa bidhaa hufanyika viwandani angalau mara moja kwa mwaka na mara baada ya zoezi hilo kaguzi za kushtukiza hufanyika mara kwa mara ili kujiridhisha kama bidhaa hizo zinazalishwa kwa Vipimo sahihi kama mzalishaji alivyobainisha katika bidhaa yake.
" Tumepita katika maduka mbalimbali yanayouza nondo kwa ajili ya ukaguzi ambapo ni zoezi endelevu linalofanyika mara kwa mara kwa lengo la kuwalinda walaji wapate bidhaa ambazo zina vipimo sahihi kulingana na thamani ya fedha wanayotoa," amesema Abdul.
Kadharika, Bw. Abdul ameeleza kuwa endapo kampuni yeyote itabainika kuwa imezalisha na kusambaza nondo zenye Vipimo ambavyo sio sahihi hatua kali za Kisheria zitachukuliwa dhidi ya mzalishaji wa bidhaa husika ikiwa ni pamoja na kutozwa faini na bidhaa zake kuzuiliwa ama kupelekwa mahakamani kwa ajili ya kutaifishwa.
Kwa upande wake Bw. Jackson Huka Mfanyakazi wa kampuni ya kamaka ambayo ni moja ya kampuni zilizofanyiwa ukaguzi amepongeza zoezi lililofanyika la ukaguzi katika bidhaa za nondo hususani katika kampuni yao kwani inaendelea kuwajengea imani wateja wao kwa kupata bidhaa zilizo sahihi kila wakati.
"Tumefurahishwa na zoezi la ukaguzi wa Vipimo katika bidhaa za nondo kwa lengo la kuwalinda wananchi ili wapate bidhaa zenye Vipimo sahihi na sisi kama kampuni inatujengea Imani kwa wateja wetu na kupelekea kutuamini zaidi katika kuwahudumia kwa kuwauzia bidhaa mbalimbali," amesema Jackson.
Wakala wa Vipimo inaendelea kutoa wito kwa wasambazaji na wazalishaji wote wa nondo kuhakikisha bidhaa wanazozalisha zinakuwa katika Vipimo sahihi kama Sheria ya Vipimo inavyo elekeza na Wananchi wasisite kutoa taarifa kwenye ofisi za WMA endapo watabaini kuwa kuna nondo hazipo katika Vipimo sahihi.
No comments:
Post a Comment