
Sehemu ya zawadi za Krismasi zilizotolewa na Mhandisi James Jumbe katika Kituo cha Wazee Kolandoto na kwa watoto wanaolelewa katika kituo cha Shinyanga Society Orphanage Centre
Na Mwandishi wetu - Malunde 1 blog
Wakati ulimwengu ukisherehekea kuzaliwa kwa Yesu Kristo, mdau wa maendeleo, Mhandisi James Jumbe, ametafsiri maana ya upendo kwa vitendo kwa kugusa mioyo ya wahitaji katika Manispaa ya Shinyanga kupitia zawadi mbalimbali za kijamii zilizolenga kuongeza furaha kwa wazee na watoto.
Katika hali ya kuonesha uungwana na ukarimu wa kipekee, Mhandisi Jumbe ametoa zawadi za Krismasi katika Kituo cha Wazee Kolandoto na kwa watoto wanaolelewa katika kituo cha Shinyanga Society Orphanage Centre , akithibitisha kuwa upendo wa kweli wa jamii upo katika namna inavyojali makundi yaliyo pembezoni.
Faraja kwa Wazee Kolandoto
Katika kituo cha Kolandoto, zawadi na mahitaji mbalimbali yamekabidhiwa kwa niaba yake na Ndg. Derick Peter, ambaye amesisitiza kuwa kuwajali wazee ni wajibu wa kijamii na si hiari.

"Mhandisi James Jumbe ameona ni vyema kurudi kwa wazee wetu ili kuwapa faraja. Heshima na matunzo kwao ni baraka kwa jamii nzima. Tumefika hapa kuhakikisha hawajihisi wapweke bali wanajiona kuwa ni sehemu muhimu ya jamii inayowathamini," amesema Derick.
Tabasamu kwa Watoto Yatima
Wakati huohuo, katika kituo cha watoto cha Shinyanga Society Orphanage Centre, zawadi hizo zimetolewa kupitia kwa msaidizi wake, Ndg. Masuka Jumbe.
Masuka ameeleza kuwa lengo kuu la Mhandisi Jumbe ni kuhakikisha watoto hao wanasherehekea sikukuu ya Krismasi kwa furaha kama watoto wengine.

"Katika kusherehekea Krismasi, Mhandisi James Jumbe ameona asiyaache nyuma makundi maalum. Ni muhimu kuwafariji na kuwapatia mahitaji ili wajione kuwa ni sehemu ya jamii yetu," amebainisha Masuka.
Mwendelezo wa Huduma kwa Jamii
Wawakilishi hao wote wawili wamethibitisha kuwa kitendo hicho si cha mara ya kwanza wala si cha mwisho, kwani Mhandisi Jumbe amekuwa na utaratibu wa kusaidia jamii ya Shinyanga kila mara.
Wamesisitiza kuwa Mhandisi Jumbe ataendelea kuwa karibu na makundi hayo ili kuwatia moyo na kuwapa mahitaji muhimu, akiamini katika kutoa kwa dhati kama njia ya kuleta mabadiliko chanya.
Nao Wazee na Watoto wamemshukuru Mhandisi Jumbe kwa kuendelea kugusa maisha yao wakisema amekuwa sehemu ya vituo hivyo.








No comments:
Post a Comment