TARURA MKALAMA YAENDELEA KUZIBORESHA BARABARA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Friday, September 20, 2024

TARURA MKALAMA YAENDELEA KUZIBORESHA BARABARA


Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) Wilaya ya Mkalama mkoani Singida inaendelea na ujenzi pamoja na matengenezo ya barabara na madaraja ili kuhakikisha wananchi wanazifikia huduma za kijamii na kiuchumi kwa urahisi.

Akiongea katika mahojiano maalum, Meneja wa TARURA katika Wilaya hiyo, Mhandisi Rahabu Thomas amesema kuwa hadi sasa miradi mbalimbali imekamilika ikiwemo ujenzi wa barabara ya Gengerankuru - Moma yenye urefu wa mita 640 kwa kiwango cha lami pamoja na kuweka taa.

Mhandisi Rahabu amesema kuwa barabara hiyo imewasaidia wananchi hasa kipindi wanapohitaji kupata huduma katika Ofisi za Serikali kwani wanafika kwa urahisi.

Aidha ameeleza kuwa mradi mwingine uliokamilika ni ujenzi wa Barabara na madaraja katika Barabara ya Iguguno - Lyelembo - Msingi yenye urefu wa Km 4.33 ambapo pia amesema kuwa barabara hiyo inarahisisha shughuli za kiuchumi kwa wananchi.

"Barabara hii ni muhimu kwa wananchi kwani sasa wanasafirisha mazao na kuzifikia huduma za kijamii kiurahisi", amesema Mhandisi Rahabu.

Naye Bi. Grace Benjamini mkazi wa kijiji cha Ilansoni amesema kuwa hapo awali mazao yao yalikosa soko la uhakika lakini kutokana na kukamilika kwa barabara hiyo sasa mazao yao yamepata soko na bei imepanda.

"Kutokana na barabara hii kupitika sasa mazao yanafika sokoni kwa urahisi na bei imeongezeka na wananchi wanapata faida", amesema.




No comments:

Post a Comment