Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro ametoa rai kwa Watanzania kuacha kuiga utamaduni wa watu wa mataifa mengine kwa kisingizio cha Haki za Binadamu.
Mhe. Ndumbaro ametoa rai hiyo, Septemba 20, 2024 katika uwanja wa Majimaji Songea mkoani Ruvuma wakati akifungua Tamasha la Tatu la Utamaduni la Kitaifa ambapo amewataka Watanzania kurithisha utamaduni kwa watoto, kuwafundisha mila na desturi za kitanzania pamoja na historia ya jamii za kitanzania.
"Familia, watu mashuhuri, watengeneza maudhui mtandaoni na taasisi za dini ziwe mstari wa mbele katika kufundisha mila na desturi na kupambana na mmomonyoko wa maadili ili utamaduni wetu uendelee kukua na kurithishwa kizazi hadi kizazi." Amesema Mhe. Ndumbaro.
Amesema utamaduni wa Tanzania unabebwa na upendo, utulivu, mshikamano, umoja, amani, utulivu pamoja na lugha adhimu ya Kiswahili ambavyo viliasisiwa na Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere wakati anaunda wizara ya Elimu na Utamaduni mwaka 1962.
Awali Mkuu wa Mkoa huo, Mhe. Kanal Ahmed Abbas Ahmed amewakaribisha washiriki wa tamasha hilo kutembelea vivutio vya utamaduni pamoja na kufurahia vyakula vya asili vya mkoa huo.
Tamasha hilo litakuwa na mashindano ya ngoma za asili na vyakula, usiku wa matumizi sahihi ya kanga, matembezi madogo, pamoja na burudani kuanzia Septemba 20 hadi 23, ambapo mgeni rasmi katika kufunga Tamasha hilo atakua Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
No comments:
Post a Comment