Waziri wa Maji Mhe. Juma Aweso (Mb) amewahakikishia wakazi wa Dar es Salaam na Pwani huduma ya maji safi na salama kwasababu changamoto ya hitilafu ya mtambo wa kuzalisha maji wa Ruvu juu tayari imerekebishwa.
Waziri Aweso amesema wakati wa ziara ya kukagua mtambo wa kuzalisha maji wa Ruvu Juu na kujionea ukarabati uliofanywa na wahandishi wa Mamlaka ya Majisafi Dar es salaam (DAWASA) baada ya kutokea hitilafu katika moja ya mitambo iliyoathiri uzalishaji wa maji safi na salama.
Amesema mtambo wa kuzalisha maji wa Ruvu juu ukiwa katika hali ya ubora wake unazalisha maji kiasi cha lita za ujazo 197 milioni kwa siku, lakini baada ya kutokea kwa hitilafu uzalishaji wa maji ulikuwa katika kiwango cha chini kiasi cha lita 170 milioni hivyo kuathiri upatikanaji wa maji katika maeneo hayo.
"Nilikuwa katika ziara ya mkoa wa Simiyu nikapata taarifa za kelele za malalamiko kuhusu kukosekana kwa maji hasa katika maeneo ya Malamba mawili, Saranga, Mbezi Msakuzi, Bonyokwa na maeneo mengine nikalazimika kumaliza ziara ili nije nijue tatizo ni nini" Aweso amesema.
Amewashukuru mafundi kutoka DAWASA kwasababu walihakikisha kuwa wanafanya kazi usiku na mchana kumaliza tatizo hilo ili wananchi waendelee kuifurahia huduma ya maji jambo ambalo tayari limeshapatiwa ufumbuzi.
Mkuu wa Wilaya ya Kibaha Nickson Simon amemshukuru Waziri Aweso kwa kutembelea katika mtambo huo na kwa sasa wamewekeza zaidi katika kuhakikisha kuwa mifugo haiathiri vyanzo vya maji na maji yanaendelea kutiririka kama kawaida.
Nickson amesema siku za karibuni wameondoa zaidi ya ng'ombe 3000 katika mto Ruvu lengo likiwa ni kukilinda chanzo hicho cha maji ili maji yaendelee kutiririka na wananchi waweze kupata maji safi na salama.
"Tumeimarisha ulinzi kwenye mto wetu wa Ruvu, juzi tuliondoa zaidi ya mifugo 3000 na tayari tumeshaandaa vyanzo vingine vya kunywesha maji mifugo yetu, lengo likiwa ni kuhakikisha wananchi wa Dar es Salaam na Pwani wanaendelea kupata maji safi na Salama." Nickson amesema.
No comments:
Post a Comment