dLAB YASHAURI WAKULIMA KUTUMIA TAARIFA ZINAZOTOLEWA NA TMA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Saturday, October 26, 2024

dLAB YASHAURI WAKULIMA KUTUMIA TAARIFA ZINAZOTOLEWA NA TMA


Na Jasmine Shamwepu, Dodoma.


WAKULIMA wameshauriwa kutumia taarifa zinazotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) kukabiliana na athari za mabadiliko tabianchi ili kuongeza tija kwenye kilimo na kuondokana na kilimo cha mazoea.

Mhadhili wa Chuo Kikuu cha Dar es Saalam (UDSM) na Mtafiti wa Mradi wa Kilimo na Data Dk. Godfrey Justo, amebainisha hayo leo  jijini hapa wakati akizungumza na waandishi wakati wa uzinduzi wa mradi huo.

Dk. Justo, amesema mradi huo ambao utatekelezwa kwa muda wa miaka miwili na Shirika la Tanzania Data Lab (d LAB) katika mikoa ya Dodoma, Manyara pamoja na Pemba ambapo walegwa ni vijana na wanawake.

Amesema, lengo la mradi huo ni kuwezesha wakulima vijana na wanawake ambao wamekuwa wakijihusisha na kilimo cha mazao ya biashara kutumia taarifa sahihi za hali ya hewa ili kukabiliana na athari za mabadiliko tabianchi.

“Lengo la mradi huu ni kuwawawezesha wakulima ambao wanalima mazao ya biashara kutumia taarifa sahihi za hali ya hewa ili kuondokana na kilimo cha mazoea na kuongeza tija kwenye kilimo na kujiongezea kipato.

“Wakulima wengi bado wanalima kwa mazoea lakini kama watawezeshwa kupata taarifa sahihi za hali ya hewa wataweza kulima kwa tija kwani watajua kiwango cha mvua katika msimu husika na kama kutakua na ukame watajipanga kupata mbegu ambazo zitakabilina na ukame”amesema

Aidha, amesema hivi sasa wakulima wengi wanalima kwa mazoea na kukariri msimu wa kilimo bila kupata taarifa sahihi za mamlaka ambazo zitawawezesha kujua msimu unaanza mwezi gani lakini pia kiwango cha mvua.

Amesema, mabadiliko tabianchi yamekuwa na tabia ya kubadili misimu na kiwango cha mvua kwa kunyesha juu ya wastani ama chini ya wastani hivyo uwepo wa taarifa za hali ya hewa ni muhimu kwa wakulima ili wajiandae kukabilina na hali hiyo.

Kadhalika, amesema mradi huo utahusisha vijana na wanawake kutokana na makundi hayo kuwa katika hatari zaidi ya mabadiliko tabianchi.

Mkurugenzi Msaidizi wa sekta za uchumi na uzalishaji Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mhandisi Enock Nyanda amesema serikali itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuweka mazingira rafiki kwa wakulima.

“Tunawashuru d LAB kwa kuleta mradi huu ambao utakwenda kusaidia wakulima vijana na wanawake kupata taarifa za hali ya hewa ili kukabiliana na athari za mabadiliko tabianchi lakini pia utakwenda kusaidia changamoto ya ajira kwa makundi haya.

“Sisi kama serikali na mamlaka ya hali ya hewa nchini TMA tutakwenda kushirikiana na wadau hawa ili kuhakikisha kuwa wakulima pamoja na wadau wengine mradi huu unakuwa na tija na kufanikiwa kwa kiasi kikubwa ili kuongeza tija kwenye kilimo biashara”amesema Nyanda

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la COSITA Tanzania la mkoani Manyara Patrice Gwasma, amesema mradi huo unakuwa msaada mkubwa kwa wakulima ambao wamekuwa wakikabiliwa na athari za mabadiliko tabianchi kwa muda mrefu.

Vile vile, amesema mradi huo utawezesha wakulima kujua hali ya hewa ili kujiandaa tofauti na ilivyo sasa ambapo wengi wao wanalima kwa mazoea na kujikuta wakipata hasara kutokana na mazao yao kufa kwa kukosa mvua za kutosha au mvua juu ya wastani.

No comments:

Post a Comment