
Na Mwandishi Wetu.
Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB) imesisitiza kuwa uhuru wa vyombo vya habari nchini upo, unalindwa kisheria na unatambuliwa katika Katiba pamoja na Sheria ya Huduma za Habari, Sura ya 229, huku ikitoa wito kwa wanahabari kuzingatia maadili na uwajibikaji katika utekelezaji wa majukumu yao.
Kauli hiyo ya JAB imetolewa na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Bodi hiyo, Wakili Patrick Kipangula, alipokuwa akizungumza katika kipindi cha moja kwa moja cha Hatua za Ushindi kinachorushwa na Kituo cha Televisheni cha Hope Channel Tanzania, leo Machi 17, 2026 jijini Dar es Salaam.
Ameeleza kuwa kifungu cha 7 cha Sheria ya Huduma za Habari kinaweka bayana haki na uhuru wa vyombo vya habari, ikiwa ni pamoja na haki ya mwandishi wa habari kutafuta, kuchakata na kusambaza taarifa, huku wananchi wakiwa na haki ya kupata taarifa sahihi kuhusu maendeleo yanayowazunguka.
“Uhuru wa vyombo vya habari upo na unalindwa kisheria. Mwandishi ana haki ya kutafuta na kusambaza taarifa, na mwananchi ana haki ya kupata taarifa. Huu ndio msingi wa uwazi na uwajibikaji katika jamii,” amesema Wakili Kipangula.
Hata hivyo, amesisitiza kuwa uhuru huo unaambatana na wajibu wa kuzingatia maadili ya taaluma, akibainisha kuwa dhana ya uwajibikaji haipaswi kuchanganywa na kile kinachoitwa ukandamizaji wa vyombo vya habari.
Amebainisha kuwa baadhi ya malalamiko ya ukandamizaji yanatokana na kutokuzingatia misingi ya kitaaluma, hususan pale ambapo taarifa zinapotolewa bila uthibitisho, uwiano au kwa lugha isiyozingatia maadili.

“Ni muhimu kutofautisha kati ya uwajibikaji na ukandamizaji. Usipozingatia maadili ya taaluma, usiseme unakandamizwa. Uwajibikaji ni sehemu ya taaluma, na haupaswi kutafsiriwa kama kubanwa kwa uhuru wa habari,” amesisitiza Kipangula.
Katika hatua nyingine, Wakili Kipangula ameeleza kuwa Serikali imeendelea kuboresha mazingira ya sekta ya habari kupitia mageuzi ya kisheria na kisera, ikiwemo kufutwa kwa Sheria ya Magazeti iliyokuwa ikitajwa kuwa kandamizi na kuanzishwa kwa Sheria ya Huduma za Habari inayolenga kuimarisha uhuru, uwajibikaji na weledi katika tasnia hiyo.
Amesema maboresho hayo yameleta mwelekeo mpya unaowezesha vyombo vya habari na wanahabari kufanya kazi zao kwa uhuru zaidi, huku wakizingatia viwango vinavyokubalika kitaaluma na kisheria.
Aidha, ametoa wito kwa wanahabari kuendelea kuilinda taaluma yao kwa kuzingatia ukweli, usahihi na uwiano katika utoaji wa taarifa, sambamba na kuheshimu haki za wananchi za kupata taarifa sahihi na kwa wakati kwa mujibu wa Sheria ya Kupata Taarifa.
Amesisitiza umuhimu kwa waajiri kote nchini kuhakikisha wanapata wataalamu wenye sifa stahiki kuingia katika menejimenti zao, sanjari na kuwatumia waandishi wenye ithibati, katika kazi zote za kihabari ili kulinda na kuipa thamani taaluma ya uandishi wa habari.

No comments:
Post a Comment