Na Veronica Mwafisi-Chato
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete amesema Serikali itaendelea kuwahudumia na kuwaenzi Viongozi wa Kitaifa Wastaafu kwa kiwango stahiki kwa mujibu wa sheria na kwa kuzingatia maelekezo ya mara kwa mara yatakayotolewa na Mamlaka.
Mhe. Kikwete ametoa kauli hiyo leo tarehe 17 Machi 2026 kwenye kumbukizi ya miaka mitano ya Rais wa Awamu ya Tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Hayati Dkt John Joseph Magufuli yaliyofanyika Chato mkoani Geita.
Amesema, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora ndiyo yenye dhamana na Matunzo ya Viongozi wa Kitaifa Wastaafu kwa Mujibu wa Hati Idhini ambayo Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan aligawa majukumu kwa Mawaziri na suala hili la kumbukizi ni mojawapo ya utekelezaji wa Sheria ya Mafao ya Hitimisho la Kazi kwa Viongozi wa Kisiasa Sura 225 jambo ambalo hata Hayati Dkt. John Joseph Magufuli, aliwahi kulitolea maelekezo.
Kwa msingi huo, tunatoa uhakika wa uendelevu wa huduma bora kwa Viongozi wa Kitaifa Wastaafu na Wajane wa Viongozi wa Kitaifa Wastaafu, amesisitiza Mhe. Kikwete.
Aidha, ameongeza kuwa Rais wa Awamu ya Tano alielekeza kuwa suala la kumbukizi linatakiwa kufanyika kwa umakini na ubora wa hali ya juu ili kuwafanya viongozi waliostaafu na wanaojiandaa kustaafu kuwa na ari ya kufanya kazi kubwa ya kulijenga Taifa wakiwa kazini kutokana na kupata uhakika wa uendelevu wa mustabali wa maisha yao na kuweka misingi bora ya kukabidhi kijiti cha uongozi wa nchi yetu.
Mhe. Kikwete amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa ruhusa na maelekezo mbalimbali kuhusu kufanyika kwa kumbukizi hiyo.
“Nikiwa ndiye Waziri mwenye dhamana na matunzo ya Viongozi wa Kitaifa Wastaafu naomba nikushukuru wewe binafsi kwa kutoa fedha za kufanikisha shughuli hii sambamba na kutusimamia katika kufanikisha jambo hili muhimu kwa Ofisi yetu, Serikali kwa ujumla na Familia ya Hayati Dkt. John Joseph Magufuli, Rais wa Awamu ya Tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo hapa inaongozwa Mama Janeth, Mjane wa Hayati Dkt. John P. J. Magufuli, ameongeza.







No comments:
Post a Comment