MAKAMU WA RAIS DKT EMMANUEL NCHIMBI, AONGOZA KUMBUKIZI YA MIAKA MITANO YA KIFO CHA HAYATI DKT. JOHN MAGUFULI - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Tuesday, March 17, 2026

MAKAMU WA RAIS DKT EMMANUEL NCHIMBI, AONGOZA KUMBUKIZI YA MIAKA MITANO YA KIFO CHA HAYATI DKT. JOHN MAGUFULI


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi amemwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kumbukizi ya miaka mitano ya kifo cha aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Hayati Dkt. John Pombe Magufuli, iliyofanyika Kilimani, Chato mkoani Geita.
 
Akitoa salamu za Serikali, Makamu wa Rais amesema ili kumuezi Hayati Magufuli kwa vitendo ni vema kila Mtanzania kujifunza wito kwa kujitoa na kufanya kazi kwa bidii. Amesema Hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, aliyejitambulisha kwa Falsafa yake ya “Hapa Kazi tu”, alitaka kila mtu kujituma na kutoa mchango wake kwa Taifa kwa njia ya kazi.  Aliamini kuwa hiyo ndiyo njia pekee inayoweza kuondoa umaskini, katika ngazi ya mtu mmoja mmoja, kaya na hata Taifa kwa ujumla.
 
Makamu wa Rais amesema katika uongozi, funzo kutoka kwa Hayati Dkt. John Pombe Magufuli ni ujasiri na uthubutu wake katika kufanya maamuzi magumu na yenye manufaa kwa Taifa. Ameongeza kwamba alifundisha umuhimu wa kuwajibika na kusimamia misingi ya haki na usawa katika kuwahudumia wananchi wote, pia hakuyumbishwa katika kupiga vita uzembe na rushwa.
 
Halidhalika, Makamu wa Rais ameongeza kwamba, Hayati Magufuli, alifundisha kuwa hatima ya Tanzania na Afrika kwa ujumla iko mikononi mwa Watanzania na Waafrika wenyewe. Akisisitiza ulinzi na matumizi ya utajiri mkubwa wa rasilimali zilizopo, kwani zinaweza kuwatoa wananchi katika umaskini. Amesema, Hayati Magufuli aliamini kuwa wajibu wa kutatua matatizo ya nchi ya kijamii, kisiasa au kiuchumi yako mikononi mwa Watanzania wenyewe.
 
Makamu wa Rais amesema katika uhai wake, Hayati Dkt. John Magufuli aliwagusa wengi kupitia utumishi na uongozi wake uliotukuka. Pamoja na mambo mengine, Mwenyezi Mungu alimjalia Hayati Dkt. John Pombe Magufuli, kipawa cha uongozi na uwezo mkubwa wa kunena na kutenda yote aliyoyaamini kuwa ya manufaa kwa Taifa na watu wake. Kila siku ya maisha yake ilijaa mafunzo kwa kila aliyemwona au kufanya naye kazi. Ameongeza kwamba, maisha yake yalikuwa ni darasa zuri kwa viongozi, na kupitia uongozi wake aliweza kulea na kuinua viongozi wapya wengi, hasa vijana.
 
Makamu wa Rais amesema, Rais Dkt. Samia Suhulu Hassan anaungana na Watanzania wote katika kumbukizi hiyo na Serikali anayoiongoza itaendelea kumuenzi Hayati Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuendeleza urathi wake.
 
Amesema Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kutambua na kuenzi mchango wa Hayati Dkt. John Pombe Magufuli, amekuwa akifuatilia kwa karibu ujenzi wa makumbusho yake iliyopo Chato na kuamua kutoa shilingi milioni 100 zilizobaki ili kukamilisha ujenzi huo.
Kumbukizi hiyo imehudhuriwa na Rais wa Zanzibar Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi ambaye amesema, namna bora katika kumuenzi Hayati Magufuli ni kuendeleza dhamira yake ya kuhimiza uwajibikaji na kuwajali wananchi hususani wanyonge na kuhakikisha rasilimali za nchi zinalindwa kwa maslahi ya Watanzania wote.
 
Amesema Hayati Magufuli alikuwa muumini mkubwa wa Muungano wa Tanzania kwa kuhakikisha wananchi wa pande zote mbili wananufaika na Muungano huo. Amesema alisimamia vema uwajibikaji na mapambano dhidi ya ufisadi na wizi wa mali za umma hatua iliyochangia kwa kiasi kikubwa katika kuimarika kwa nidhamu katika utumishi wa umma na kulinda rasilimali za umma.
 
Ameupongeza uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa jitihada za kusimamia, kuendeleza na kuhakikisha maono na malengo ya Hayati Magufuli yanatimizwa kwa vitendo.
 
Rais Dkt. Mwinyi, ametoa wito kwa Watanzania kumuenzi Hayati. Magufuli kwa kuendelea kutekeleza azma yake ya kudumisha tunu ya amani ili iendelee kuwa msingi wa mafanikio kiuchumi na kijamii. Vilevile amewahimiza Viongozi wa Dini, kuendelea kuliombea Taifa amani.
 
Akizungumza kwa niaba ya familia ya Hayati Dkt. John Magufuli, Mbunge wa Viti Maalum Mhe. Jesca Magufuli, amesema kama familia katika kumbukumbu za Hayati Dkt. Magufuli, wanamkumbuka kama mmoja ya Viongozi aliyobeba kwa uzito mkubwa jukumu la kuimarisha misingi ya maendeleo ya Taifa.
 
Ameishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa namna inavyoendelea kuhifadhi kumbukumbu za Hayati Dkt. Magufuli kwa heshima na staha inayostahili.
 
Aidha familia imempongeza na kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa ushirikiano aliyoutoa kwa familia katika kipindi chote cha miaka mitano pamoja na kuendeleza kazi za Hayati Dkt. Magufuli za ujenzi wa Taifa kwa kutambua kwamba historia ya Taifa lolote hujengwa na vizazi vilivyopokea wajibu kutoka kwa waliotangulia na kuendeleza safari ya maendeleo.
 
Katika Kumbukizi hiyo, jumla ya kiasi cha shilingi milioni 474 ikiwemo ahadi na fedha taslimu zimekusanywa katika harambee iliyoongozwa na Makamu wa Rais Dkt. Emmanuel Nchimbi kwa lengo la kumalizia ujenzi wa Kanisa Katoliki Parokia ya Kilimani Wilayani Chato.

No comments:

Post a Comment