
Na Okuly Julius _Dodoma
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Mhe William Lukuvi amevitaka vyama vya siasa nchini kuhamasisha wananchi kujiandikisha kwenye daftari la wapiga kura kwa ajili ya Uchaguzi wa serikali za mitaa na kujitokeza kupiga kura na kuchagua viongozi watakao Tatua changamoto mbalimbali kwenye maeneo yao.
Lukuvi ameyasema hayo jijini Dodoma kwenye Kikao cha dharura cha Baraza la Vyama vya Siasa ambapo amesema yupo tayari kuwa daraja la maendeleo kwa kupokea ushauri na maono ya viongozi wa vyama vyote vya siasa na kuwasilisha serikalini.
Amesema kuwa kila kiongozi wa chama cha siasa ni kiongozi na mpenda maendeleo hivyo watumie fursa hiyo kuendesha vyama vyao kwa njia sahihi
“Leo rasmi nimekuja kujitambulisha kwenu kwamba ni mwenzenu tupo pamoja katika siasa, tufanye siasa njema yenye madhumuni ya kudumisha amani, maelewano na maendeleo kwasababu vyama ni njia tu ya kwenda popote,”
Na kuongeza kuwa “Nia yangu siyo kuja kwenu tu, nia yangu ni kufungua milango kwamba hata humu serikalini kwetu sisi mnaweza mkaja kwani najua si masuala ya siasa tu wakati mwengine vipo vyama ambavyo vinapenda kutoa ushauri hata baada ya uchaguzi kutoa ushauri kwa serikali.” amesema Lukuvi
Aidha Lukuvi amesema viongozi wa vyama huwa wana maono ya kutoa ushauri na maoni mbalimbali ya maendeleo kwa serikali hivyo mlango wa kuwasilisha hayo maoni na ushauri upo kwake.
Sambamba na hayo Lukuvi amesema kikao hicho cha dharura kitakuwa na umuhimu kuelekea katika uchaguzi wa serikali za mitaa pamoja na chaguzi zingine kwani kitasaidia hali ya Siasa kuwa shwari kuelekea kwenye uchaguzi.
Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa NCCR MAGEUZI Joseph Selasini bhui amesema Mkutano huo wa dharura ni wa kwanza kufanyika katika kipindi ambacho wanajipanga kuelekea kwenye uchaguzi wa serikali za mtaa.
"tunampongeza Msajili wa Vyama vya siasa kwa ubunifu huu wa kuwakutanisha viongozi wa vyama vya siasa na kujadili agenda moja tu ya hali ya Siasa nchini kabla ya uchaguzi ila kusaidiana katika kuwahamasisha wananchi kujiandikisha na kujitokeza katika uchaguzi, jambo hili hata Dunia itaona nia njema ya kutaka kuona uchaguzi unakuwa huru na haki, "ameeleza Selasini








No comments:
Post a Comment