MAKAMU WA PILI WA RAIS WA ZANZIBAR MHE. HEMED SULEIMAN ABDULLA AWATAKA MAAFISA KUKUMBUKUMBU NA NYARAKA KUTIMIZA WAJIBU WAO - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Thursday, October 31, 2024

MAKAMU WA PILI WA RAIS WA ZANZIBAR MHE. HEMED SULEIMAN ABDULLA AWATAKA MAAFISA KUKUMBUKUMBU NA NYARAKA KUTIMIZA WAJIBU WAO

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Hemed Suleiman Abdulla akipokea zawadi wakati wa mkutano mkuu wa 12 wa Chama cha Kitaaluma cha Menejimenti ya Kumbukumbu na Nyaraka Tanzania (TRAMPA) kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan iliyotolewa na Chama hicho kwa kutambua mchango anaoutoa katika taaluma hiyo.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Hemed Suleiman Abdulla akifungua mkutano mkuu wa 12 wa Chama cha Kitaaluma cha Menejimenti ya Kumbukumbu na Nyaraka Tanzania (TRAMPA) katika Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete jijini Dodoma.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene akitoa neno la utangulizi kabla ya kumkaribisha Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Hemed Suleiman Abdulla (hayupo pichani) kufungua mkutano mkuu wa 12 wa Chama cha Kitaaluma cha Menejimenti ya Kumbukumbu na Nyaraka Tanzania (TRAMPA) jijini Dodoma.

Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bw. Juma Mkomi akitoa utambulisho wa Viongozi wa Serikali waliohudhuria ufunguzi wa mkutano mkuu wa 12 wa Chama cha Kitaaluma cha Menejimenti ya Kumbukumbu na Nyaraka Tanzania (TRAMPA) uliofanyika jijini Dodoma.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene (wa kwanza kushoto) akifurahia jambo na Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais-UTUMISHI na Utawala Bora, Bw. Xavier Daudi wakati Waziri huyo alipowasili katika Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete kuhudhuria ufunguzi wa mkutano mkuu wa 12 wa Chama cha Kitaaluma cha Menejimenti ya Kumbukumbu na Nyaraka Tanzania (TRAMPA) jijini Dodoma.

Sehemu ya washiriki wa mkutano mkuu wa 12 wa Chama cha Kitaaluma cha Menejimenti ya Kumbukumbu na Nyaraka Tanzania (TRAMPA) wakiwa kwenye ufunguzi wa mkutano huo uliofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete jijini Dodoma.

Baadhi ya Wakurugenzi Wasaidizi na Watumishi wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora wakiwa kwenye ufunguzi wa mkutano mkuu wa 12 wa Chama cha Kitaaluma cha Menejimenti ya Kumbukumbu na Nyaraka Tanzania (TRAMPA) jijini Dodoma.

Baadhi ya Watunza Kumbukumbu kutoka Ofisi ya Rais-UTUMISHI na Utawala Bora wakisikilza hotuba ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Hemed Suleiman Abdulla wakati akifunga mkutano mkuu wa 12 wa Chama cha Kitaaluma cha Menejimenti ya Kumbukumbu na Nyaraka Tanzania (TRAMPA) uliofanyika jijini Dodoma.


Na Mwandishi Wetu _Dodoma


Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Hemed Suleiman Abdulla amewataka Maofisa Kumbukumbu na Nyaraka kutimiza wajibu wao kwa kufanya kazi kwa kuzingatia Sheria, Taratibu na Kanuni huku akiwataka kutunza siri za Serikali kwa kutozitoa nje ya ofisi zao.

Ametoa kauli hiyo wakati akimwakilisha Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi katika Mkutano wa 12 wa Chama cha Kitaaluma cha Menejimenti ya Kumbukumbu na Nyaraka Tanzania (TRAMPA) unaofanyika kwa muda wa siku nne Jijini Dodoma

Amesema maofisa hao ni watu muhimu sana ikizingatiwa kuwa Serikali kila inapotaka kufanya maamuzi yeyote katika kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo hurejea kwenye kumbukumbu na nyaraka zilizotunzwa.

‘‘Nimemsikiliza Mwenyekiti wenu ametaja changamoto mbalimbali zinazowakabili katika kutekeleza majukumu yenu, kutokana na unyeti wa kazi yenu napenda kuwaahidi kuwa tutaendelea kuzitatua kwa kadri ya uwezo wetu ili kuhakikisha mnatoa huduma bora katika maeneo yenu ya kazi.

Aidha, Mhe. Abdulla ameipongeza TRAMPA kwa kuendelea kubaki kwenye misingi ya uanzishwaji wake na hivyo kuwa msaada kwa wanachama hao katika kupaza sauti kwa Serikali juu ya changamoto zao ili ziweze kupatiwa suluhu.

Kwa upande wake Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene amesema Serikali itaendelea kuajiri Maofisa Kumbukumbu na Nyaraka ili kupunguza changamoto ya upungufu wa maofisa hao.

Aidha, Mhe. Simbachawene amekitaka chama hicho kutumia fursa ya uwepo wake kupaza sauti katika masuala mbalimbali yanayohusu kada yao ili kuboresha zaidi utendaji kazi.

"Serikali iliridhia muunde TRAMPA ili muwe wamoja katika kupaza sauti kwenye maeneo yanayowahusu, hivyo tumieni fursa hiyo kufikisha ujumbe ili ufanyiwe kazi kwa wakati," amesisitiza Mhe. Simbachawene.

Naye Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Mhe. Haroun Ali Suleiman amesema yeye na Waziri mwenzake wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene wanafanya kila liwezekanalo kuhakikisha suala la maslahi kwa Maofisa Kumbukumbu na Nyaraka linashughulikiwa ili yaendane na majukumu ya kazi wanayoifanya.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Joseph Mhagama amesema kukutana kwa Maofisa Kumbukumbu na Nyaraka katika mkutano huo utawawezesha kubadilishana uzoefu na ujuzi utakaoisaidia Serikali katika kutimiza azma ya kuwahudumia wananchi kwa ukamilifu na taifa kwa ujumla.

"Wana TRAMPA ninaamini mmekutana hapa kwa lengo la kupeana mbinu za kuboresha na kuimarisha utendaji kazi hivyo niwasihi mkitoka hapa mkatoe huduma bora zaidi ya awali ili kuhakikisha Serikali inapiga hatua kubwa za kimaendeleo kupitia kada yenu," amesisitiza Mhe. Dkt
Mhagama

Naye Mwenyekiti wa TRAMPA, Bi. Devotha Mrope amesema utunzaji wa kumbukumbu na nyaraka ni muhimu kwa Serikali na Sekta binafsi kwani unasaidia kupata mrejesho wa masuala mbalimbali wa wapi tulipotoka na tunapoelekea katika kuimarisha utendaji kazi na maendeleo ya nchi.

Akizungumzia mafanikio ya chama hicho, Bi. Mrope amesema TRAMPA imekuwa jicho kwa wanataaluma katika kuzisemea changamoto zinazowakabili ikiwemo kuwekewa mazingira bora ya kufanyia kazi, motisha, kutambuliwa na kuthaminiwa.

Bi. Mrope amesema utunzaji wa kumbukumbu nyaraka umeimarika kutokana na kuimarishwa kwa mafunzo mbalimbali ya kitaaluma katika kada hiyo ambapo kasi ya uvujaji wa siri umepungua kwa kiasi kikubwa tangu chama hicho kilipoasisiwa.

No comments:

Post a Comment