Prof. Ng’umbi awahimiza wananchi kuchangamkia fursa za elimu - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Wednesday, October 2, 2024

Prof. Ng’umbi awahimiza wananchi kuchangamkia fursa za elimu

Sehemu ya washiriki wakifuatilia wasilisho wakati wa semina ya siku moja ya wadau wa kukuza mafunzo ya ufundi kwa vijana wenye ulemavu wa akili iliyofanyika Oktoba 1, 2024 Ofisi za Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima mtaa wa Bibi Titi Mohamed jijini Dar es Salaam.
Mkuu wa Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima, Prof. Michael Ng’umbi akiongea wakati wa semina ya wadau wa kukuza mafunzo ya ufundi kwa vijana wenye ulemavu wa akili iliyofanyika Oktoba 1, 2024 Ofisi za Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima mtaa wa Bibi Titi Mohamed jijini Dar es Salaam.
Mwakilishi wa Balozi wa Finland nchini, Bwana Tomi Lounio akifungua semina ya wadau wa kukuza mafunzo ya ufundi kwa vijana wenye ulemavu wa akili iliyofanyika Oktoba 1, 2024 Ofisi za Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima mtaa wa Bibi Titi Mohamed jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi wa Elimu Maalum wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dkt. Magreth Matonya akifunga semina ya wadau wa kukuza mafunzo ya ufundi kwa vijana wenye ulemavu wa akili kwa niaba ya Kamishna wa Elimu Oktoba 1, 2024, Ofisi za Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Maendeleo ya Wanawake na Vijana la Mafiga (Mafiga Women and Youth Development Organization – MWAYODEO), Dkt. Venance Mlali (katikati) akimtambulisha Mwakilishi wa Balozi wa Finland nchini, Bwana Tomi Lounio kwa Mkuu wa Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima, Prof. Michael Ng’umbi alipowasili katika Ofisi za taasisi hiyo Oktoba 1, 2024.
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Maendeleo ya Wanawake na Vijana la Mafiga (Mafiga Women and Youth Development Organization – MWAYODEO), Dkt. Venance Mlali akiwasilisha matokeo ya utekelezaji wa mradi wa mafunzo ya stadi za ujuzi kwa vijana wenye ulemavu wa akili wakati wa semina ya wadau iliyofanyika Oktoba 1, 2024 Ofisi za Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima jijini Dar es Salaam.
Mwakilishi wa Balozi wa Finland nchini, Bwana Tomi Lounio (katikati) na Mwakilishi wa Kamishna wa Elimu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dkt. Magreth Matonya (wa pili kushoto) wakiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya washiriki wa semina ya wadau wa kukuza mafunzo ya ufundi kwa vijana wenye ulemavu wa akili iliyofanyika Oktoba 1, 2024 Ofisi za Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima jijini Dar es Salaam.

Na Mwandishi Wetu Dar es Salaam 

Mkuu wa Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima (TEWW), Prof. Michael Ng’umbi amewataka wananchi kuzitumia fursa mbalimbali za elimu zinazotolewa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na wadau kwa maendeleo yao na taifa.

Kiongozi huyo ameyasema hayo wakati wa semina ya siku moja ya wadau wa kukuza mafunzo ya ufundi kwa vijana wenye ulemavu wa akili iliyofanyika Oktoba 1, 2024 Ofisi za Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima mtaa wa Bibi Titi Mohamed jijini Dar es Salaam.

Miongoni mwa fursa hizo, kwa mujibu wa Prof. Ng’umbi ni mafunzo ya stadi za ujuzi kwa vijana wenye ulemavu wa akili yanayoratibiwa na Shirika lisilo la Kiserikali la Maendeleo ya Wanawake na Vijana la Mafiga (Mafiga Women and Youth Development Organization – MWAYODEO), na Mpango wa Elimu Changamani kwa Vijana walio nje ya mfumo rasmi (IPOSA) unaoratibiwa na TEWW.

Akiongea katika semina hiyo, Mwakilishi wa Kamishna wa Elimu ambaye pia ni Mkurugenzi wa Elimu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dkt. Magreth Matonya amesema kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania haitamwacha mtoto yeyote akose elimu.

“Serikali imejipanga kwenda mkoa kwa mkoa kuwabaini watoto wote wenye changamoto ili kuwapatia elimu ya stadi za ujuzi,” Dkt. Matonya amesema, na kuongeza kuwa “hadi sasa Tanzania ina jumla ya vyuo 10 vya watu wenye ulemavu vinavyowezesha watoto wote wenye changamoto kuhudumiwa.”

Kwa upande wake, Mwakilishi wa Balozi wa Finland nchini, Bwana Tomi Lounio ameahidi kwamba nchi yake itaendelea kushirikiana na Serikali ya awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika miradi mbalimbali ya elimu, hususan elimu jumuishi kwa sababu eneo hilo ni miongoni mwa vipaumbele vyao.

Katika wasilisho lake kuhusu Mradi wa Mafunzo ya Stadi za Ujuzi kwa Vijana wenye Ulemavu wa Akili, Mkurugenzi Mtendaji wa MWAYODEO, Dkt. Venance Mlali amesema kuwa mradi huo umefanikiwa kutoa mafunzo kwa jumla ya vijana 181 wenye ulemavu wa akili (151 kutoka Manispaa ya Morogoro, na 30 kutoka Mji wa Ifakara).

Pia, mradi huo umeweza kubaini vijana zaidi ya 300 wenye ulemavu wa akili mkoani Morogoro, umewajengea uwezo baadhi ya walimu katika vyuo vya ufundi kufundisha vijana wenye ulemavu wa akili, na umechangia kuongeza hamasa na ari ya wazazi kuwapatia vijana wenye ulemavu wa akili fursa ya kupata elimu ya ufundi.
Kwa mujibu wa Dkt. Mlali stadi za ujuzi zinazotolewa na shirika lake kwa sasa ni pamoja na: upishi, ushonaji, ufyatuaji matofali, ufumaji, uashi, ufugaji kuku, bustani na useremala.

Mradi huo ulioanza kutekelezwa miaka minne iliyopita unafadhiliwa na Serikali ya Finland kupitia jumuiya ya Vaaasa Tanzania.

No comments:

Post a Comment