WATANZANIA WAASWA KUZINGATIA AFYA ZAO KWA KUWA NA LISHE BORA. - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Wednesday, October 30, 2024

WATANZANIA WAASWA KUZINGATIA AFYA ZAO KWA KUWA NA LISHE BORA.


Moreen Rojas,
Dodoma.

Mkurugenzi Msaidizi Huduma za lishe kutoka Wizara ya Afya Neema Joshua Mwapili ametoa Rai Kwa watanzania kuzingatia afya zao Kwa kuwa na lishe Bora kwani itasaidia kuondokana na upungufu wa madini kwenye miili yetu.

Ameyasema hayo jijini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maadhimisho ya siku ya lishe kitaifa oktoba 30,2024.
Aidha ameongeza kuwa kazi yao ni Kuhamasisha wananchi wanakula kinachofaa Kwa ajili ya afya zao hivyo kama Wizara wanashirikiana na Mamlaka nyingine pamoja na wadau wa lishe kuhakikisha wanahudumia jamii kwani suala la lishe ni la kijamii zaidi.

"Siku ya lishe ilizinduliwa rasmi 2020 jijini Dodoma lengo ni kuhamasisha jamii na kuleta nguvu Kwa pamoja"

Kwa upande wake Stella Kimambo Afisa lishe ambaye anafanya kazi na shirika la chakula na kilimo la umoja wa mataifa (FAO) Tanzania  amesema siku ya lishe ni muhimu Kwa kuweza kijitathmini kama taifa tumefikia wapi kwenye suala zima la lishe.

"Watanzania lazima tujitathimini je ni sahihi tunachokula,kwani tuna miongozo ya chakula watoto watapewa kiasi gani?hivyo wataalam waache kupotosha jamii Kwa kutumia miongozo ya nje ya nchi ambayo haiendani na miongozo ya Tanzania"

Aidha ameongeza kuwa mtoto anapaswa kupewa vyakula mchanganyiko ili kuboresha afya yake,pamoja na kuepuka kuwapa watoto vyakula vilivyosindikwa na kuwapa vyakula vya asili.

"Tunawasihi watanzania kutumia muongozo uliotolewa na Wizara ya Afya Tanzania bara pamoja na visiwani kwani ulaji wa bara na visiwani ni tofauti"

Sanjari na hayo Waziri wa Afya,Jenista Mhagama ameziagiza halmashauri zote nchini, kuhakikisha fedha za kutekeleza afua za lishe , ikiwemo uongezaji wa virutubishi kwenye vyakula, uhamasishaji na elimu ya lishe kwa jamii na tathimini ya hali ya lishe, ili kubaini matatizo ya utapiamlo zinatumika kama ilivyokusudiwa.

Waziri Mhagama ametoa agizo hilo  jijini Arusha, wakati akiongea na waandishi wa habari, kuhusu maadhimisho ya siku ya Lishe Kitaifa yanayoadhimishwa Oktoba 30 kila mwaka,  yenye kauli mbiu isemayo "Mchongo ni Afya yako,zingatia unachokula" 

Amesema endapo kila halmashauri zikitenga fedha hizo, zitawezesha kusaidia jamii kupata elimu na uelewa zaidi  ngazi ya kata,mashuleni, ili kupunguza tatizo la utapiamlo na kupata jamii bora kwa maendeleo ya kiuchumi na kijamii .

Pia amesema jamii bado inakabiliwa na changamoto ya utapiamlo wa aina nyingi, ikiwemo ukondefu,udumavu, uzito pungufu hususan kwa watoto , utapiamlo wa upungufu wa vitamini na madini mwilini, yaani njaa iliyofichika , upungufu wa damu, utapiamlo wa lishe ya kuzidi ,kiribatumbo pamoja na magonjwa yasiyoambukiza.

"Utapiamlo hudhoofisha makuzi ya watoto kimwili na kiakili,ikiwemo kuongeza hatari ya magonjwa na kutuletea  gharama kubwa za matibabu kwani serikali inatenga shilingi bilioni tano  kila mwaka, katika taasisi za afya kwaajali ya kupambana na magonjwa yasiyoambukiza ikiwemo sukari,figo,moyo,shinikizo la damu, "amesema.

Ameongeza kuwa utapiamlo hudhoofisha makuzi ya watoto kimwili na kiakili kuongeza hatari ya magonjwa na  kukosa ubunifu, uwezo wa kufanya maamuzi wakati wa utu uzima, hivyo ni vizuri  kuchukua hatua za makusudi kwa kufanya maamuzi sahihi kila siku ya kula  aina bora za vyakula na kufanya mazoezi.

Aidha  ametoa tahadhari kwa jamii kupunguza hatari ya kupata utapiamlo wa lishe ya kuzidi  na magonjwa yasiyoambukiza katika jamii, kama vile kisukari,shinikizo la juu la damu, magonjwa ya moyo,kiharusi na magonjwa ya figo , hivyo muhimu kushirikiana na serikali kuhamasisha jamii ulaji unaofaa na matumizi ya vyakula vilivyoongezwa virutubishi kupitia majukwa mbalimbali.

Amesema kwa mujibu wa takiwmu za Taasisi ya  Moyo Jakaya Kikwete (JKCI)  inaonyesha kila mwaka watoto 1500 wanapatikana na matatizo ya moyo na kuhitaji kufanhiwa upasuaji hali inayoleta  gharama kubwa zinazowashinda   wazazi wengi na kusababisha  serikalli  kusaidia kuchangia matibabu hayo.

No comments:

Post a Comment