WAANDISHI WA HABARI NGUZO MUHIMU KATIKA UTEKELEZAJI WA SHERIA YA ULINZI WA WATOA TAARIFA NA MASHAHIDI - BI. MHANDO - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Monday, October 27, 2025

WAANDISHI WA HABARI NGUZO MUHIMU KATIKA UTEKELEZAJI WA SHERIA YA ULINZI WA WATOA TAARIFA NA MASHAHIDI - BI. MHANDO


Kaimu Mkurugenzi Idara ya Katiba na Ufuatiliaji Haki, Wizara ya Katiba na Sheria Bi. Aksa Mhando,akizungumza leo Oktoba 27,2025 jijini Dodoma, wakati wa ufunguzi wa kikao kazi cha siku mbili kilichoandaliwa na Wizara hiyo , kilicholenga kuwajengea uelewa waandishi wa habari kuhusu sheria hiyo pamoja na Kanuni zake zilizotangazwa kupitia Tangazo la Serikali Na. 59 la Februari 10, 2023.


Na OKULY JULIUS, OKULY BLOG, DODOMA


Waandishi wa habari wametajwa kuwa nguzo muhimu katika utekelezaji wa Sheria ya Ulinzi wa Watoa Taarifa na Mashahidi, Sura ya 446, kwa kuwa wao ndio daraja kuu kati ya Serikali na wananchi katika kueneza elimu, kuhamasisha uwajibikaji na kulinda misingi ya utawala bora.

Kauli hiyo imetolewa jijini Dodoma na Kaimu Mkurugenzi Idara ya Katiba na Ufuatiliaji Haki, Wizara ya Katiba na Sheria Bi. Aksa Mhando, wakati wa ufunguzi wa kikao kazi cha siku mbili kilichoandaliwa na Wizara hiyo , kilicholenga kuwajengea uelewa waandishi wa habari kuhusu sheria hiyo pamoja na Kanuni zake zilizotangazwa kupitia Tangazo la Serikali Na. 59 la Februari 10, 2023.

Ambapo Bi. Mhando amesema vyombo vya habari vina nafasi ya kipekee katika kuhakikisha wananchi wanaelewa haki zao, wajibu wao, na namna ya kutoa taarifa au ushahidi kwa usalama na ujasiri.

“Vyombo vya habari ni sauti ya wananchi na daraja la mawasiliano kati ya Serikali na jamii. Kupitia ninyi, elimu kuhusu Sheria ya Ulinzi wa Watoa Taarifa na Mashahidi inaweza kuwafikia Watanzania wote, kuwahamasisha kutoa taarifa za uhalifu bila woga, na kujenga imani katika mifumo ya haki,” amesema Bi.Mhando

Ameongeza kuwa Sheria hiyo ni nyenzo muhimu katika mapambano dhidi ya rushwa, uhalifu na ukiukwaji wa haki za binadamu, kwa sababu inalinda watu wanaojitokeza kutoa taarifa au ushahidi dhidi ya makosa mbalimbali.

“Sheria hii inatoa ulinzi wa kisheria, kiusalama na kijamii kwa wale wanaojitokeza kwa ujasiri kufichua matendo maovu. Ni hatua kubwa katika kuimarisha utawala wa sheria na uwajibikaji nchini,” amefafanua.

Aidha, ameeleza kuwa waandishi wa habari mara nyingi hupokea taarifa nyeti kutoka kwa watu wanaofichua uhalifu, hivyo ni muhimu kufahamu utaratibu sahihi wa kisheria wa kushughulikia taarifa hizo ili kulinda usalama wa watoa taarifa.

Kupitia kikao hicho, washiriki wamepata nafasi ya kujadili namna bora ya kuandaa mikakati ya utoaji elimu kwa umma kuhusu sheria hiyo, na kuhamasisha wananchi kushiriki katika mapambano dhidi ya uhalifu bila kuogopa madhara.

“Kanuni hizi zimefafanua utaratibu wa kuwapa motisha wale wanaotoa taarifa zinazookoa mali za umma au kusaidia kukamatwa kwa wahalifu. Pia zimeweka taratibu za kuwafidia wanaoathirika kutokana na taarifa walizotoa,” ameongeza.

Wizara ya Katiba na Sheria imesisitiza kuwa elimu kwa umma kuhusu sheria hiyo ni muhimu kwa kuwa itasaidia wananchi kuelewa kuwa taarifa wanazotoa zitabaki siri na zitashughulikiwa kwa usalama mkubwa.

“Tunatarajia mkakati mtakaoandaliwa utasaidia vyombo vya habari kutoa elimu sahihi kwa wananchi kuhusu umuhimu wa sheria hii, ili jamii iwe na uelewa mpana na utayari wa kushiriki katika kulinda haki, usalama na amani nchini,” amesema.








No comments:

Post a Comment