
Wizara ya Nishati imeanza kutoa elimu kuhusu Nishati Safi ya Kupikia
kwa Maafisa Dawati wa Nishati Safi ya Kupikia ngazi ya mikoa na
halmashauri kwa lengo la kuwa na uelewa wa pamoja katika utekelezaji
wa Mkakati wa Taifa wa Nishati Safi ya Kupikia pamoja na kuwawezesha
Maafisa Dawati kutambua majukumu yao katika utekelezaji wa mkakati..
Akifungua mafunzo hayo, wilayani Kibaha mkoani Pwani, Mwakilishi wa
Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani, Bi. Hadija Mruma ameipongeza Wizara
ya Nishati kwa jitihada mbalimbali inazochukua kwa vitendo katika
kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia nchini mojawapo ikiwa
ni kuhakikisha elimu na vifaa vya nishati safi ya kupikia vinafika
hadi ngazi za Mikoa, Halmashauri na Vijiji.
Ameeleza kuwa Mkoa wa Pwani unachukua hatua mbalimbali kuhakikisha
kuwa wanachi wanatumia nishati safi ya kupikia katika ngazi ya
taasisi, kaya n.k akitoa mfano kuwa asilimia 76 ya taasisi zinazolisha
watu zaidi ya 100 mkoani humo zimeshahamia kwenye nishati safi ya
kupikia.
Aidha, amewapongeza Watendaji wa Wakala wa Nishati Vijijini ( REA)
ambao wanashirikiana na Mkoa wa Pwani kuhamasisha matumizi ya nishati
safi ya kupikia ikiwemo utoaji mitungi ya gesi kwa bei ya ruzuku.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Nishati Safi ya Kupikia
kutoka Wizara ya Nishati, Bw. Ngereja Mgejwa ameeleza kuwa mafunzo
kuhusu Nishati Safi ya Kupikia yameanza kutolewa wilayani Kibaha,
mkoani Pwani kwa kuhusisha Mikoa ya Pwani, Morogoro, Dar es Salaam,
Mtwara, Lindi na Tanga.
Ameongeza kuwa, elimu ya nishati safi ya kupikia itaendelea kutolewa
kwa Maafisa Dawati wa Nishati Safi ya Kupikia katika mikoa mingine
iliyosalia kwani lengo ni kutoa elimu husika katika Mikoa yote 26
pamoja na Halmashauri zake.
Amesema kuwa suala la matumizi ya nishati safi ya kupikia ni
kipaumbele cha nchi na dunia kwa ujumla ili kuondokana na athari zake
katika mazingira, afya na kiuchumi.
Naye, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano kutoka Wizara ya Nishati, Bi.
Neema Mbuja ameeleza kuwa mafunzo yanayotolewa kwa maafisa dawati hao
yanahusisha pia masuala ya Mkakati wa Taifa wa Mawasiliano wa Nishati
Safi ya Kupikia.
Ameeleza kuwa ili kufikisha elimu kwa wananchi kuhusu nishati safi ya
kupikia ni muhimu maafisa dawati hao wakafahamu njia za mawasiliano
zitakazowasadia kufikisha elimu na jumbe zitakazotumika kuendana na
maeneo wanayoyasimamia.
Ameongeza kuwa uwepo wa Mkakati wa Taifa wa Mawasiliano wa Nishati
Safi ya Kupikia (National Clean Cooking Communication Strategy)
unatoa mwongozo wa namna wadau watakavyoshirikiana kutoa elimu kwa
umma ili kuondoa dhana potoshajii (misconception) kuhusu nishati safi
ya kupikia na kubadili mitazamo hasi kuwa chanya kwa lengo la kuleta
mabadiliko katika utekelezaji wa ajenda ya kitaifa ya nishati safi ya
kupikia.

No comments:
Post a Comment