WAZIRI SIMBACHAWENE AIPONGEZA SHULE YA SEKONDARI KINYEREZI KWA KUIBUA NA KUKUZA VIPAJI VYA WANAFUNZI - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Saturday, October 12, 2024

WAZIRI SIMBACHAWENE AIPONGEZA SHULE YA SEKONDARI KINYEREZI KWA KUIBUA NA KUKUZA VIPAJI VYA WANAFUNZI


Waziri Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. George Simbachawene ameipongeza Shule ya Sekondari Kinyerezi ya jijini Dar es Salaam kwa 
kuwalea wanafunzi kwa mrengo wa kisasa hali inayopelekea kuibua na kukuza vipaji vingi miongoni mwa wanafunzi hao huku akiwataka wanafunzi hao kuwa na nidhamu ili kunufaika na vipaji vyao.

Amesema katika dunia ya sasa kwenye sanaa ndiko kuna uwanja mkubwa wa ajira

Mhe.Simbachawene ametoa kauli hiyo leo Oktoba 12, 2024 wakati akizungumza kwenye mahafali ya 15 ya kidato cha nne katika Shule ya Sekondari Kinyerezi iliyopo katika Wilaya ya Ilala jijini Dar es Salam 

" Nimefarijika kuona vipaji vya kila aina, nimewaona wasanii wenye vipaji vikubwa na pia nimeambiwa kuna mwanafunzi kwa sasa yupo Uingereza alichukuliwa tu mara baada ya kuhitimu masomo yake kutokana kipaji kikubwa alichonacho cha kucheza mpira " amesema Mhe.Simbachawene 

Amesema makuzi ya mrengo wa kisasa kwa wanafunzi wa sasa ni jambo lisiloepukika kwa vile wanafunzi walio wengi wanaohitimu masomo yao hawarudi vijijini kulima 

Kufuatia hatua hiyo Mhe.Simbachawene amewataka wahitimu hao wa kidato cha nne na wanafunzi wanaoendelea na shule licha ya vipaji walivyonavyo wajitahidi kusoma kwa bidii huku akiwasisitiza kujiepusha kuiga tamaduni za kigeni ambazo haziendani na tamaduni zetu.

Katika hatua nyingine, Mhe.Simbachawene amempongeza Rais Mhe.Samia Suluhu Hasssan kwa kukubali kutoa kiasi cha Sh. Bilioni 28 kwa ajili ya jiji la Dar es Salaam ili ziweze kutumika kwenye ujenzi wa madarasa

Amesema Serikali ya awamu ya tano imedhamiria kuhakikisha wanafunzi wanapata elimu kwenye mazingira bora na ya kisasa ili kuhakikisha hakuna mtoto anayeachwa nyuma katika kutimiza ndoto zake

Awali, Mkuu wa Shule hiyo, Daniel Mwaka amesema Shule hiyo licha ya kuwa nyumba ya vipaji lukuki lakini kwenye suala la ufaulu wa masomo imekuwa ifanya vizuri mwaka hadi mwaka
  
Amesema katika kipindi cha miaka mitatu mfululizo, ufaulu wa wanafunzi umekuwa ni zaidi ya asilimia 80 na kusisitiza kuwa ufaulu wa wahitimu wa mwaka huu ufaulu utapanda zaidi hadi kufikia asilimia 93 kutokana na jinsi wanafunzi hao walivyoandaliwa.

No comments:

Post a Comment