Na Ashrack Miraji, Vunjo Kilimanjaro.
Iddy Hussein Mfinanga, aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa ACT Wazalendo Jimbo la Vunjo, ajiunga na Chama Cha Mapinduzi (CCM)
Iddy Hussein Mfinanga, gwiji wa siasa za upinzani kutoka jimbo la Vunjo, amekihama chama cha ACT Wazalendo na kujiunga rasmi na Chama Cha Mapinduzi (CCM). Mfinanga, ambaye aligombea ubunge kupitia ACT Wazalendo katika uchaguzi wa 2020, alifanya uamuzi huo rasmi katika uzinduzi wa kampeni za uchaguzi wa serikali za mitaa uliofanyika leo, tarehe 20 Novemba 2024, katika kata ya Njia Panda, jimbo la Vunjo.
Katika tukio hilo, Mfinanga aliendelea kusema kuwa nimeamua kuungana na chama cha serikali ili kuongeza mchango wangu katika maendeleo ya taifa. Alisema, “Ni ukweli usiopingika kuwa kwa kipindi chote cha uongozi wa Mama Samia, kuna mambo mengi yamefanyika kwa nguvu kubwa sana. Kama nchi, ni muda wa kuunganisha nguvu ili tusonge mbele zaidi.”
Aidha Mfinanga Alisema CCM si Chama kibaya
Akiwa mbele ya umati wa wananchi na wanasiasa wa CCM, Mfinanga alifafanua sababu za uamuzi wake wa kuhamia CCM. Alisema, “Vyama ni platform zinazotumiwa kufikisha michango yetu kwa jamii. Ukiona kwamba mchango wako hauelekei vizuri katika chama kimoja, na unaona nafasi nyingine itakayosaidia taifa lako zaidi, basi ni busara kuchukua hatua hiyo.” Aliongeza kuwa, licha ya kwamba aliaminishwa kuwa CCM ni chama kibaya, amekutana na watu wema ndani ya chama hicho, na kusema kuwa “ubaya unawezekana kukutana na mtu mmoja mmoja, siyo chama chote. Hata vyama vya upinzani kuna watu wabaya, lakini hiyo siyo taswira ya chama.”
Aahidi Kuendelea Kutumikia Jamii
Mfinanga aliahidi kuendelea kutoa mchango wake kwa jamii, akisema, “Mambo niliyokuwa nikifanya kwa jamii yangu, nitaendelea kuyaendeleza kwa nguvu zaidi. CCM ni chama kinachothamini watu wanaofanya kazi kwa bidii na kukuza maendeleo. Hakuna chama kinamkataa mtu anayekisaidia kukipa jina zuri kwenye jamii.”
Alisema kuwa anakubaliana na sera za CCM na kwamba, kama kiongozi mwenye uwezo, atatumia fursa hiyo kufanya kazi zaidi kwa manufaa ya wananchi. “Sioni CCM itanizuia kuleta mchango chanya, bali itaniunga mkono. Nitaendelea kufanya kazi kubwa kwa ajili ya kata yangu ya Makuyuni (Himo), jimbo la Vunjo, mkoa wa Kilimanjaro na taifa kwa ujumla,” alimalizia Mfinanga.
Pia, katika uzinduzi huo, vijana wengi walijitokeza kuachana na vyama vyao vya awali ACT na CDM na kujiunga na CCM, wakishirikiana na Mfinanga katika kuleta mabadiliko. Walipokelewa na viongozi wa CCM wa ngazi za wilaya, mkoa, na taifa, huku wakionyesha kuunga mkono uamuzi wa Gwiji la siasa Mfinanga na kutaka kushirikiana naye katika kukuza maendeleo ya taifa.
No comments:
Post a Comment