
Na Mwandishi Wetu - Dodoma
Kesi Tatu zinazowakabili watuhumiwa wa kesi ya uhaini kutokana na vurugu za Oktoba 29,2025 zimesikilizwa Machi 11,2026 kwenye Mahakama ya Hakimu mkazi, Dodoma mbele ya Hakimu mkazi Mkuu Mhe. Dennis Mpelembwa dhidi ya watuhumiwa Sebastian Mbiligwa, George Ambrosi, Meshaki Andrea na Juma Pius.
Ambapo jopo la Mawakili wa serikali liliongozwa na wakili wa serikali Chuwa na huku upande wa utetezi ukiwa na mawakili kutoka Chama Cha wanasheria Tanganyika (TLS) na Kituo Cha Sheria na haki za binadamu (LHRC) kliniki ya Dodoma ukiongozwa na wakili Sofia Gabriel na Ibrahimu Mcharo.
Kesi hizo ni kesi ya jinai namba 28515 ya mwaka 2025 yenye kosa moja la kuchoma Ofisi ya Kata ya Mbabala iliyowahusu washtakiwa wote watano,
Kesi ya jinai namba 28518 ya mwaka 2025 yenye kosa la kuchoma nyumba ya Bi. Paskazia Mayala na kuchoma gari la Bw. Thomas Mzile huko kata ya mbabala mkoani Dodoma, inayowahusu washtakiwa Sebastian Mbiligwa, George Ambrose na Salma Abdallah.
Kesi ya Jinai namba 28703 ya mwaka 2025 inayowahusu washtakiwa wote watano yenye shtaka la shambulio la kudhuru mwili mashauri yote yalipokuja mbele ya Hakimu Mkazi mkuu kusikilizwa, Mwendesha mashtaka amefanya makubaliano ya mkataba wa kukiri kosa (Plea bargaining agreement) na washtakiwa Watatu kati ya Watano kwenye kesi zote tatu yaani George Ambrose, Meshack Andrea na Juma Pius, Mahakama imeyakubali makubaliano hayo na kuwaachia huru bila masharti yoyote wala kulipa fidia ama kuwa na rekodi za kijinai washtakiwa hao watatu kwa pamoja.
Katika kesi ya uhaini na kula njama za kutenda kosa kesi ya jinai namba 28637 ya mwaka 2025 iliyokuwa ikiwakabili washtakiwa wote watano, Mwendesha mashtaka kwa mamlaka aliyonayo chini ya kifungu Cha 92(1) cha Sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai Sura ya 20 Marejeo ya 2023 ameonesha nia ya kutoendelea kuwashtaki (Nolle Prosequi) watuhumiwa hao 3 (George, Meshaki na Juma) na hivyo kuachiwa huru.
Kesi zote tatu zimepangwa kuja kuendelea kusikilizwa tarehe 16 Machi katika Mahakama ya Hakimu mkazi, Dodoma mbele ya Hakimu mkazi Mkuu Mhe. Mpelembwa kwa washtakiwa wawili waliobaki (Sebastian na Salma) ambao ni familia Moja yaani mke na mume.
Ikumbukwe pia siku hiyo ni siku ya shauri la uhaini ambapo litakuja kwa kutajwa mbele ya Mhe. Mpelembwa na kwa sasa idadi ya watuhumiwa katika kesi zote Nne ni watuhumiwa wawili tu.

No comments:
Post a Comment