📌 Ni wakati akitoa mchango Bungeni kuhusu Mpango wa Taifa wa Maendeleo
📌 Ataja kuongezeka kwa kiasi cha umeme katika Gridi ya Taifa
📌 Aeleza usambazaji umeme vijijini ulivyofanyika kwa mafanikio; Vijiji 78 Tu vyasalia
📌 Aeleza jitihada zilizofanyika Sekta ya Mafuta na Gesi Asilia; Utoaji wa Leseni na Duru ya Tano ya kunadi vitalu
📌 Asema Sekta ya Nishati ipo salama chini ya Dkt.Biteko
Naibu Waziri wa Nishati, Mhe Judith Kapinga amesema mafanikio yanayoonekana katika Sekta ya Nishati ni jitihada za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Dkt. Samia Suluhu Hassan kwani ndiye anayetafuta fedha za kutekeleza miradi ya nishati nchini.
Mhe. Kapinga ameyasema hayo Novemba 07, 2024 Bungeni jijini Dodoma wakati akitoa ufafanuzi wa hoja mbalimbali zilizotolewa na Wabunge wakati wa mjadala wa mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa mwaka wa fedha 2025/2026.
"Miradi mingi inatekelezeka kwa sababu ya jitihada za Mheshimiwa Rais, huku Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko akihakikisha kwamba miradi yote inatekelezwa kwa ufanisi na weledi mkubwa. Amesema Kapinga
Ameongeza kuwa, Sekta ya Nishati ina umuhimu mkubwa nchini kwani ni sekta wezeshi katika kuchangia ukuaji wa uchumi kupitia biashara, viwanda, kilimo pamoja na shughuli nyingine za kijamii.
Kapinga amesema katika kipindi chote cha utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo Sekta ya Nishati imejikita katika kuhakikisha inaboresha miundombinu ya uzalishaji, usafirishaji na usambazaji wa umeme pamoja na kuboresha misingi ya kiuchumi katika sekta ya mafuta na gesi ikiwa ni pamoja na kuboresha mazingira wezeshi kwa kuhusisha sekta binafsi.
Amesisitiza kuwa wakati wa kuanza utekelezaji wa Mpango wa Taifa mwaka 2021 Nchi ilikuwa na megawati 1,571 za umeme kwenye gridi ya Taifa lakini utakapokamilika mradi wa umeme wa Julius Nyerere Nchi itakuwa na megawati 3,914.
Amesema mradi wa Julius Nyerere hivi sasa unazalisha megawati 940 kupitia mitambo minne na kuongeza kuwa ili kuwa na umeme mwingi zaidi Serikali inaangalia vyanzo vingine vya uzalishaji wa umeme.
Kapinga ameongeza kuwa, Serikali inatekeleza miradi mingine ya uzalishai umeme ikiwemo Malagarasi 49.5 MW, Kakono 87.8 MW pamoja na mradi wa kuzalisha umeme wa Jua wa Kishapu Shinyanga utakaozalisha meagawati 150 ambao ujenzi wake umeanza.
Ameeleza kuwa, Serikali ya Awamu ya Sita inayo azma na nia ya kuhakikisha utekelezaji wa miradi ya uzalishaji wa umeme inaendelea.
Akizungumzia uzalishaji umeme kwa kutumia Jotoardhi, Mhe. Kapinga amesema Tanzania inakadiriwa kuwa na vyanzo vyenye uwezo kuzalisha takriban megawati 5,000 na kuongeza kuwa, Serikali inayo nia ya kuanza kuzalisha umeme kwa kutumia Jotoardhi.
Amesema tayari maeneo matano yameshabainishwa kwa ajili ya kupata Nishati ya Jotoardhi ikiwemo Ruhoi, Natron, Mbozi, Songwe na Kiejo-Mbaka.
"Mheshimiwa Rais ametoa fedha takriban shilingi bilioni 15.7 kwa ajili ya kununua mitambo ya uchorongaji maeneo haya ambayo tumeyabaini yana rasilimali ya jotoardhi." Amesisitiza Mhe. Kapinga
Kuhusu Nishati Jadidifu amesema mwelekeo wa Serikali ya Awamu ya Sita ni kuendeleza zaidi vyanzo vya nishati jadidifu ili kupunguza utegemezi wa kiuchumi, kuongeza usalama wa nishati na kuleta uendelevu wa kinishati ambao unachangia kiasi kikubwa katika kulinda mazingira.
Amesema pamoja na miradi ya uzalishaji umeme Serikali pia inawekeza katika miradi mbalimbali ya usafirishaji umeme ya msongo mkubwa na mdogo ambapo baadhi ya miradi inayotekelezwa itaiunganisha Tanzania na Nchi jirani.
Ameitaja baadhi ya miradi inayoiunganisha Tanzania na Nchi jirani kuwa ni mradi utakaoiunganisha Tanzania na Nchi nane za Ukanda wa Jangwa la Sahara pamoja na mradi unaoiunganisha Tanzania na Nchi 14 za ukanda wa Afrika Mashariki.
Kuhusu usambazaji wa umeme vijijini, Mhe. Kapinga amesema mwaka 2021 Serikali ilitoa takriban shilingi Trilioni 1.753 kuhakikisha umeme unapelekwa kwenye Vijiji vyote na vimebaki vijiji 78 kukamilisha vyote.
Amesema kwa sasa Serikali iko kwenye utekelezaji wa mradi wa Vitongoji kwa kuanza na Vitongoji 3,070 na mradi mwingine ni wa kupekeka umeme kwenye vitongoji 4000.
Ameongeza kuwa, azma ya Serikali kati miaka mitano hadi saba ni vitongoji vyote 32,000 ambavyo vimebakia viwe vimekamilika.
Kwa upande wa Sekta ys Gesi amesema nia ya Serikali ni kuona mradi wa LNG unaendelea na utakapokamilika utazalisha takribai futi za ujazo trilioni 45.
Kuhusu miradi ya mafuta na gesi kwa mkondo wa juu, kati na mkondo wa chini amesema baada ya miaka 16 Serikali imetoa leseni ya kuendeleza kitalu cha Ruvuma Ntorya chenye jumla ya futi za ujazo trilioni 1.4.
Amesisitiza kuwa baada ya takriban miaka 12 Serikali inaenda kwenye duru ya tano ya kunadi vitalu vya mafuta na gesi asilia ifikapo mwezi Machi 2025.
" Nia yetu ni kuhakikisha vitalu vyetu 24 ambavyo 21 vipo katika bahari kuu na vitatu vipo Ziwa Tanganyika tunafaya matumizi mazuri ya rasilimali ambazo tunazo, tutahakikisha tunatumia rasilimali tulizonazo za mafuta na gesi kwa faida ya Taifa letu." Ameeleza Mhe. Kapinga
Kuhusu kutumia gesi asilia kwa ajili ya uzalishaji wa mbolea, Mhe. Kapinga amesema Serikali inao mpango kabambe kwa ajili ya matumizi ya gesi wa 2017 hadi 2046, ambao umejikita katika kuwezesha viwanda kutumia gesi asilia katika uzalishaji na uzalishaji wa mbolea inayotokana na Nishati hiyo.
No comments:
Post a Comment