MABORESHO YA BANDARI YA TANGA YALIVYOLETA MANUFAA KIUCHUMI - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Sunday, November 10, 2024

MABORESHO YA BANDARI YA TANGA YALIVYOLETA MANUFAA KIUCHUMI


Na: Dk. Reubeni Lumbagala


Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) ni taasisi muhimu nchini ikiwajibika kusimamia na kutoa huduma bora za bandari pamoja na kuhamasisha matumizi na kuendeleza miundombinu yake.

Bandari za Dar es Salaam, Tanga na Mtwara ndizo Bandari kubwa Tanzania na zote zikiwa katika Bahari ya Hindi. Tanzania pia ina bandari katika Ziwa Victoria, Ziwa Nyasa na Ziwa Tanganyika mbali na babdari ndogo za kwenye bahari kama Bandari ya Lindi, Pangani na Bagamoyo, ambazo zote ziko chini ya TPA.

Kwa mujibu wa Sheria ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Na. 17 ya mwaka 2004, Bandari zote nchini zinapaswa kuwa chini ya TPA na mana ya "Bandari" eneo lolote kwenye mwambao wa bahari, ziwa, au mto ambako shughuli za upakiaji na upakuaji wa mizigo na abiria hufanyika. Yapo mengi yamefanyika katika kuboresha Bandari za Tanzania zikiwemo za kwenye maziwa lakini makala hii itajikita zaidi kuhusu Bandari ya Tanga.

Unapozungumzia maendeleo ya Mkoa wa Tanga kamwe huwezi kuacha kuzungumzia mchango wa Bandari hii kutokana na kuwa moyo wa uchumi wa Tanga. Lakini pia mchango wa Bandari hii unagusa nchi nzima kwani makusanyo yanayopatikana katika Bandari ya Tanga yanaingizwa katika makusanyo ya Taifa na hivyo kutumika kuboresha na kukuza maendeleo ya nchi nzima na si mkoa wa Tanga pekee.

Mbali na kuhudumia mkoa wa Tanga, Bandari hii pia inahudumia mikoa ya jirani ya Arusha, Manyara, Mara, Pwani, Singida na hata nchi maeneo ya nchi jirani za Kenya na Uganda. Kutokana na umuhimu wa kuongeza mapato kupitia Bandari hii, serikali imekuwa ikiiboresha kwa kuifanya ya kisasa zaidi ili kupakia na kupakua mizigo mingi kwa muda mfupi.

Taarifa zilizopo zinaonesha kwamba katika siku za karibuni serikali iliwekeza shilingi bilioni 429.1 katika kufanya maboresho kwenye Bandari ya Tanga.

Uwekezaji huu ulihusisha kuongeza kina cha maji kutoka mita tatu hadi mita 13, kupanua njia ya meli kugeuza na kuijengea uwezo wa bandari kupakua mizigo kutoka meli kubwa ndani ya siku mbili, tofauti na siku tano au zaidi hapo awali kabla ya maboresho. Vilevile, uwekezaji umewezesha ununuzi wa vifaa vipya vya kupakua mizigo na kupanua gati mbili hadi kufikia upana wa mita 450.

Meneja wa Bandari ya Tanga, Masoud Mrisha anakiri kuwa uwekezaji uliofanyika katika Bandari ya Tanga una manufaa makubwa. “Sasa tuna uwezo wa kushughulikia meli kubwa zaidi kuliko hapo awali. Pamoja na maboresho haya, meli sasa zinaweza kuja moja kwa moja kwenye gati hizo ambayo ni mabadiliko makubwa kutoka kwa hali ya awali ambapo meli zililazimika kufunga kwenye kina cha umbali wa kilomita 1.7 nje ya gati (na hivyo mizigo kupakuliwa kwa kutumia maboya maalumu ambayo pia huitwa matishari).” amesema Mrisha. Kutokana na maboresho haya makubwa, Bandari ya Tanga sasa ina uwezo wa kupokea meli nyingi na kubwa kwa wakati mmoja hali inayochechemua ongezeko la mapato na ukuaji wa uchumi wa nchi.

Kwa mujibu wa Mrisha, wakati wa robo ya kwanza ya mwaka wa fedha wa sasa, Bandari ya Tanga imeshahudumia jumla ya tani 333,643 za mizigo, ikipita lengo lake la tani 283,225 kwa asilimia 17.“Hii ni uboreshaji mkubwa kulinganishwa na tani 204,000 zilizohudumiwa katika kipindi kama hicho mwaka wa fedha wa 2023/2024. Kwa ujumla Bandari ya Tanga ilishughulikia tani 1,191,480 za mizigo wakati wa mwaka mzima wa fedha wa 2023/2024, ikiongezeka kutoka tani 890,901 mwaka uliopita. Aidha, Bandari imefanikiwa kuhudumia meli 113 wakati wa robo ya kwanza, ikipita lengo lake la kuhudumia meli tano tu.” amesisitiza Mrisha.

Haya ni mageuzi na mapinduzi makubwa yaliyofanyika ambapo Serikali ya Awamu ya Tano iliyokuwa ikiongozwa na Hayati Dk. John Pombe Magufuli ilianza mchakato wa maboresho ya Bandari hii, lakini Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Dk. Samia Suluhu Hassan ikaendeleza kazi hiyo nzuri, na ndiyo maana tunaona matunda ya uwekezaji mkubwa wa bilioni 429.1.

Mafanikio mengine yaliyopatikana katika kipindi cha miezi mitatu ya robo mwaka wa fedha 2024/2025 ni kuongezeka mapato kutoka shilingi bilioni 11 ambayo Bandari ya Tanga ilipangiwa hadi kufikia bilioni 18.6. Haya ni matokeo ya ongezeko la meli zinazoitumia Bandari hii ya Tanga ambapo wingi wa meli unachochea wingi wa mapato yanayokusanywa.

Kwa mfano; meli kubwa kampuni ya Seafront Shipping Services Limited ilitia nanga huku ikiwa imebeba shehena yenye bidhaa mchanganyko yakiwemo magari makubwa ya mizigo zaidi ya 350. Afisa Uhusiano wa TPA nchini, Enock Bwigane amesema kampuni ya Seafront Shipping Services Limited imeshaleta meli 12 kutoka China ambazo zimehudumiwa na Bandani ya Tanga.

UMMY MWALIMU.

Mbunge wa Jimbo la Tanga Mjini kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Ummy Ally Mwalimu amekuwa mstari wa mbele kupigania maboresho ya Bandari hii kutokana na umuhimu wake katika kuchagiza maendeleo ya wananchi wake wa Tanga Mjini na nchi kwa ujumla.

Mwaka 2018, Rais wa Awamu ya Tano Hayati Dk. John Magufuli akiwa katika ziara ya uwekaji wa jiwe la Msingi la Bomba la Mafuta eneo la Chongoleani, Tanga Mjini, alipokea ombi maalum kutoka kwa Ummy Mwalimu, juu ya kuiboresha Bandari ya Tanga. Ombi hilo la Ummy Mwalimu lilikubaliwa na Rais Mafuguli.

Vilevile, nakumbuka katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2020, Ummy Mwalimu aliipa kipaumbele Bandari ya Tanga kutokana na kuelewa mnyororo mkubwa wa thamani uliopo endapo Bandari hiyo itazidi kuboreshwa. Hivyo aliahidi endapo atachaguliwa kuwa Mbunge wa kuchaguliwa Jimbo la Tanga Mjini, ataishawishi serikali kuifanyia maboresho makubwa Bandari hiyo.Baada ya kumalizika uchaguzi wa mwaka 2020, Serikali ya Awamu ya Tano ilianzisha mchakato wa kuiboresha Bandari ya Tanga na vilevile Serikali ya Awamu ya Sita ikaendeleza mchakato huo na sasa bilioni 429.1 zimeshatumika katika kuifanya Bandari ya Tanga kuwa ya kisasa zaidi.

Maboresho ya Bandari ya Tanga yameenda sambamba usajili wa Chama Cha Madereva wa Transit Mkoa wa Tanga (CHAMATTA). Usajili wa chama hiki ambacho mlezi wake ni Ummy Mwalimu kinaongeza fursa ya ajira za madereva wa malori ya mizigo ambapo kutokana na wingi wa meli kubwa za mizigo zinazotia nanga katika Bandari ya Tanga, madereva hawa wanapata fursa ya kusafirisha bidhaa na mizigo ndani na nje ya nchi.

Aidha, Bandari ya Tanga imefungua fursa ya ajira kupitia ongezeko la kampuni nyingi zilizosajiliwa kufanya kazi na Bandari ya Tanga na hivyo kuongeza fursa za ajira. “Awali tulikuwa tunafanya kazi na makampuni ya clearing agent 32 na baada ya maboresho, yameongezeka makampuni mengine 132, hivyo tuna jumla ya makampuni 164.” amesema Mrisha.

Mafanikio ya Bandari ya Tanga yanachangia pia ukuaji wa sekta ya kilimo na uvuvi. Wakulima kutoka wilaya mbalimbali za mkoa wa Tanga kama vile Lushoto, Handeni, Korogwe, Kilindi Muheza na wilaya nyingine katika mikoa mingine nchini wataweza kuuza mazao yao kama vile katani, matunda na mbogamboga nje ya nchi kupitia usafirishaji wa mazao hayo Bandarini. Pia, wavuvi wa Tanga wanaweza kusafirisha samaki kwenda nje ya nchi na hatimaye kukuza vipato vyao na nchi pia.

Mnyororo mwingine wa thamani kupitia maboresho ya Bandari ya Tanga ni pamoja na ukuaji wa sekta ya biashara. Hii ni kutokana na ukweli kuwa wawekezaji na wafanyabiashara watakaofikia Tanga wataweza kununua bidhaa za Tanga, watakula na kulala katika hoteli za Tanga. Watapata huduma za usafiri kupitia pikipiki maarufu bodaboda, watapanda daladala na Taxi za mkoa wa Tanga na hivyo kukuza uchumi wa Tanga na nchi.Sekta ya viwanda pia inakwenda kukua kwani wawekezaji watavutiwa kufungua viwanda vipya na kupanua vilivyopo ili kuongeza uzalishaji kutokana na uhakika wa usafirishaji wa bidhaa zao ndani na nje ya nchi kupitia Bandari hii.

Hivyo basi, Bandari ya Tanga ni fursa kwa wawekezaji na wafanyabiashara kutoka ndani na nje ya nchi kufungua viwanda Tanga kutokana na usafiri bora na wa uhakika wa majini. Wawekezaji na wafanyabiashara karibuni Tanga.Kwa hakika, uwekezaji wa bilioni 429.1 katika Bandari ya Tanga umeleta matokeo chanya kwa mkoa wa Tanga na nchi kwa ujumla hasa katika nyanja ya uchumi.

Wanaosema Tanga ni lango kuu la uchumi kwa nchi za Afrika Mashariki hawajakosea kwani uwekezaji, maboresho na mapinduzi makubwa yaliyofanyika katika Bandari ya Tanga yanafanya kauli hiyo kuwa ya kweli na si ndoto za mchana. Kama ikiwezekana maboresho yaendelee na kuongeza gati zaidi ili kuzidi kushindana na Bandari ya nchi jirani ya Mombasa.

Mwandishi ni Mwalimu wa Shule ya Sekondari Mlali iliyoko wilaya ya Kongwa mkoani Dodoma.

Maoni: 0620 800 462.

No comments:

Post a Comment