Na Mwandishi Wetu-Rukwa
Naibu Waziri, Menejimenti ya Utumishi wa Umma ma Utawala Bora Mhe.Deus Sangu amesisitiza umuhimu wa Wananchi wa Jimbo la Kwela kushiriki kikamilifu katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa huku akibainisha kuwa uchaguzi huu ni fursa kwa wananchi kupata viongozi wa karibu wanaojua changamoto zinazowakabili za moja kwa moja katika maeneo yao.
Mhe.Sangu ambaye pia ni Mbunge wa Kwela ametoa kauli hiyo mapema leo Jumatano Novemba 27, 2024 mara baada ya kumaliza kupiga kura katika Kitongoji cha Pokopoko Kata ya Laela Mkoani Rukwa
Akiwa ameonesha kuridhika na idadi ya wapiga kura waliojitokeza katika kitongoji hicho na jinsi mchakato wa uchaguzi unavyoendelea, Mhe.Sangu amewataka Wananchi waliobaki kutimiza haki yao ya kikatiba kwa kujitokeza kupiga kura.
Amesisitiza kuwa ushiriki wa kila raia ni muhimu katika kuhakikisha mchakato wa uchaguzi unafanikiwa kwa haki na uwazi, huku akiwapongeza wale ambao tayari wamepiga kura kwa kuwa mfano mzuri wa uzalendo.
No comments:
Post a Comment