📌 Kapinga asema lengo ni kuchochea kasi ya ukuaji wa Elimu
📌 Aweka Jiwe la Msingi ujenzi wa nyumba ya Mwalimu Shule ya Mbungani
📌 Asema miradi ya maendeleo itawafikia wananchi wote bila kuangalia umbali
Naibu Waziri wa Nishati ambaye pia ni Mbunge wa Vijana Mkoa wa Ruvuma (CCM), Mhe.Judith Kapinga ameahidi kutoa kompyuta 139 katika Shule za Msingi 139 zilizopo Halmashauri ya wilaya ya Mbinga Vijijini ili kuchochea kasi ya ukuaji wa Elimu katika wilaya hiyo.
Mhe. Kapinga ametoa ahadi hiyo Novemba 28, 2024 wakati wa hafla ya uwekaji wa Jiwe la Msingi kwenye ujenzi wa Nyumba ya Mwalimu katika Shule ya Msingi Mbungani iliyopo Halmashauri ya wilaya ya Mbinga Vijijini.
"Nitatoa kompyuta 139 ifikapo Januari 2025 ili zitumike katika Shule za Msingi 139 zilizopo Halmashauri ya Wilaya Mbinga Vijijini kwa lengo la kuendelea kuchochea kasi ya ukuaji wa maendeleo ya Elimu nchini." Amesema Mhe. Kapinga
Aidha, pamoja na kuweka Jiwe la Msingi la ujenzi wa nyumba ya Mwalimu katika Shule ya Msingi Mbungani wilayani Mbinga, Mhe.Kapinga amechangia fedha ili kuongeza nguvu katika ujenzi wa nyumba hiyo.
Akizungumza na Wazee wa Kijiji cha Kindimbajuu katika Halmashauri hiyo, amesema kuwa Serikali inaendelea na hatua za utekelezaji wa miradi ya maendeleo ikiwemo usambazaji wa umeme kwenye Vitongoji ili kuhakikisha huduma hiyo inawafikia Watanzania wote bila kujali umbali aliopo mwananchi.
No comments:
Post a Comment