TANROADS YATEKELEZA AGIZO LA BASHUNGWA, YAFUNGA MIZANI KUPIMA UZITO WA MAGARI - TUNDUMA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Thursday, November 21, 2024

TANROADS YATEKELEZA AGIZO LA BASHUNGWA, YAFUNGA MIZANI KUPIMA UZITO WA MAGARI - TUNDUMA


Wakala ya Barabara (TANROADS) imefunga mizani inayohamishika (mobile weighbridge) ya kudhibiti uzito wa magari katika eneo la Tunduma kwa ajili ya kupima magari yanayotoka Tunduma kuelekea Dar es Salaam ili kupunguza msongamano wa malori yanayosubiria kwa muda mrefu kupima uzito katika mzani mmoja wa Mpemba unaotoa huduma mpakani mwa Tanzania na Zambia.

Ufungaji wa Mizani hiyo ni utelelezaji wa maelekezo ya Serikali yaliyotolewa na Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa Novemba 18, 2024 wakati alipokagua na kujionea msongamano wa malori katika eneo hilo ambalo lilitegemea mzani mmoja wa Mpemba.

Akizungumza baada ya kukamilisha zoezi hilo, Meneja wa TANROADS Mkoa wa Songwe, Mhandisi Suleiman Bishanga amesema juhudi hizo ni matokeo ya maelekezo yaliyotolewa na Serikali inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kurahisisha ufanyaji biashara kupitia huduma ya usafirishaji.

"Waziri Bashungwa alitoa maagizo ya kutafuta suluhisho la haraka, na kwa kushirikiana na TANROADS Mkoa wa Mbeya, tumefanikisha kupunguza msongamano mkubwa uliokuwa ukisababisha usumbufu kwa madereva hapa Tunduma," alisema Mhandisi Bishanga.  

Mhandisi Bishanga amesema TANROADS kwa Kushirikiana na Jeshi la Polisi wanaendelea kuimarishaji ukaguzi na upimaji wa magari kupitia mfumo wa mizani ya kupima magari yakiwa kwenye mwendo (weigh in motion) ambapo zoezi hilo linasaidia kupunguza msongamano wa magari kusubilia kwa muda mrefu.

Aidha, Mhandisi Bishanga amesema kazi ya ujenzi wa kituo cha maegesho katika eneo la Chimbuya unaendelea kwa kasi ikiwa ni mikakati endelevu ya kupunguza msongamano katika barabara hiyo.

Katika nyakati tofauti, Madereva wa Malori wameishukuru Serikali kwa kuendelea kufanyia kazi changamoto ambazo wamekuwa wakikabiliana nazo barabarani hususani katika eneo la Tunduma.

No comments:

Post a Comment