MAENEO YALIYOATHIRIKA NA MVUA KUBWA DODOMA KUREJESHEWA MAJI NDANI YA SAA 72 - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Saturday, December 7, 2024

MAENEO YALIYOATHIRIKA NA MVUA KUBWA DODOMA KUREJESHEWA MAJI NDANI YA SAA 72


Na Gideon Gregory, Dodoma.


Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dodoma (DUWASA), imesema kufuatia uharibifu wa miundombinu ya maji uliotokea katika baadhi ya maeneo katika jiji la Dodoma watahakikisha huduma hiyo inarejeshwa ndani ya masaa 72 hususani katika Mtaa wa Meriwa Kata Ipagala.

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa DUWASA leo Disemba 7,2024 Fundi Sanifu kutoka katika Mamlaka hiyo Kelvin Swai amesema wamejipanga kwa dharura ili kuweza kuhakikisha huduma inarudi mapema kwa wateja.

"Kwasasa mafundi wapo kazini wanaendelea na mapambano kuhakikisha huduma inarejea kwa haraka kwa wateja, pia kuna maeneo mengine kama Meriwa ambapo kuna bomba limesombwa na maji kwenye daraja ambapo mafundi wetu wanaendelea na matengenezo yote hii ni kuhakikisha huduma inarejea kwa uharaka,"amesema. 

Pia ameongeza kuwa changamoto hiyo imeweza kuleta hasara kwa taasisi ila wamejipanga kwaajili ya dharura kama hizo ili zisiendelee kusababisha madhara zaidi kwa wananchi na kupelekea kukosa huduma ya maji.

Mvua hiyo imepelekea wananchi walioko katika maeneo yaliyothirika kukosa huduma maji kwa takribani siku tatu jambo lililopelekea wananchi kuiangukia DUWASA ili waweze kurejeshewa huduma kama ilivyokuwa hapo awali.

"Kwakweli tunaiomba DUWASA pamoja na Serikali waweze kutusikiliza siku ya tatu sasa hatuna maji bomba limekatika hapa mtaani kwetu, lakini tunaamini ujio wao leo utakuwa na neema kubwa kwetu,"wamesema.

Wakati huo huo pia DUWASA imesema changamoto ya maji inayoukumba Mtaa wa Swaswa Mnarani Kata ya Ipagala jijini Dodoma itaenda kutatulika hivi karibuni kutokana na mikakati ambayo tayari wamejiwekea kwani yapo baadhi ya maeneo yanapata na mengine yanakosa huduma hiyo.

"Katika eneo hili kumekuwa kuna baadhi ya maeneo wateja wamekuwa wakikosa maji na kama DUWASA kuna utaratibu na mkakati ambapo mmoja wapo kuna mradi ulifanyika eneo la Mlimwa C ambao lengo lake ni kutatua kero ya maji ya wananchi wa eneo hilo na hapa tulipo leo mtandao ulianzishwa kule ambao upo kwaajili ya kusambaza maji,"amesema. 

Imesema tayari wamesikiliza kero za wateja wao na ndani ya wiki mbili changamoto hiyo itakuwa imetatulika na huduma itakuwa inapatikana vizuri.

No comments:

Post a Comment