🌍✳️Kila wilaya imetengewa majiko 3,255
Mkuu wa mkoa wa Singida, Mhe. Halima Dendego, tarehe 05 Desemba, 2024 amepokea majiko ya gesi yapatayo 19,530 kutoka kwa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) yenye thamani ya shilingi milioni 406 katika hafla ya iliyofanyika kwenye Ofisi yake ambapo amesema, Singida imejiandaa kuyasambaza majiko hayo pamoja na kutoa elimu ya nishati safi ya kupikia, mapema mwezi Januari, 2025.
Mhe. Dengego amesema, majiko hayo ya gesi yamekuja katika wakati sahihi kwa kuwa Wananchi wengi waliiomba Serikali pamoja na Wadau mbalimbali kupata majiko hayo kwa njia ya ruzuku ili wayanunue kwa wingi kwa ajili ya matumizi yao ya kila siku.
“Tunawashukuru REA kwa kutuletea majiko ya gesi kupitia msambazaji (Lake Gas) Wananchi wa mkoa wa Singida wayanunue ili kuendelea kutumia teknolojia za nishati safi ambapo katika mkoa wetu, ni asilimia 20 tu ndiyo wanatumia majiko ya gesi na umeme. Jambo hili litafanya Wananchi wetu watunze mazingira pamoja na kulinda afya zao kutokana na madhara yatokanayo na matumizi ya nishati chafu”. Amesema Mhe. Dendego.
“Tunamshuruku Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzaia, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwa Wananchi wamekuwa wakituuliza ni lini?, tutawaletea teknolojia za kisasa za nishati safi tena kwa bei ya ruzuku, hatukuwa na majibu. Mradi huu, umetupa majibu ya kuwajibu Wananchi”. Alimalizia, Mkuu wa mkoa Singida, Mhe. Dendego.
Kwa upande wake, Mhandisi Mwandamizi wa Miradi kutoka REA, Deusdedith Malulu amesema, fursa ya kupata jiko la gesi la kilo sita (6) ni ya kila Mwananchi wa mkoa wa Singida na kuongeza kuwa sharti la kupata jiko hilo ni Kitambulisho cha Taifa au namba ya NIDA pamoja shilingi 20,000 amezitaja wilaya zitazonufaika na Mradi huo ni pamoja na wilaya ya Ikungi, Iramba, Itigi, Manyoni, Mkalama na Singida.
“Kila wilaya, itapelekewa majiko ya gesi 3,255 pamoja na vichomeo vyake (Burners) kupitia kampuni LAKE GAS Limited Ltd. Tunaendelea kuhamasisha kuhusu matumizi ya nishati safi ili wajitokeze kwa wingi ili wanunue kwa bei ya punguzo ya asilimia 50”. Amesema, Mhandisi, Malulu.
Wakati huo huo, Mhandisi Malulu amemueleza Mkuu wa mkoa Singida kuwa REA imeleta fursa ya mkopo na nufuu wa ujenzi wa vituo vidogo vya bidhaa za mafuta vijijini yaani (Diseli na Petroli) ambapo kila Mwananchi mwenye nia ya kutaka kujenga kituo kidogo cha mafuta vijijini, anaweza kuomba mkopo wenye riba nafuu pamoja na ukomo wa miaka saba na kuongeza kuwa shilingi milioni 133 zinakopeshwa kwa ajili ya ujenzi wa kituo kimoja cha mafuta.
Mhandisi Malulu ameongeza kuwa masharti ya kupata mkopo huo ni nafuu na kwamba masharti ya mkopo huo pamoja fomu za maombi, zinapatikana kwenye tovuti ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kwa anwani ya www.rea.go.tz
No comments:
Post a Comment