"SERA MPYA YA ELIMU KUZALISHA WAHITIMU WENYE UJUZI NA MAARIFA "- MSIGWA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Wednesday, January 29, 2025

"SERA MPYA YA ELIMU KUZALISHA WAHITIMU WENYE UJUZI NA MAARIFA "- MSIGWA




Na Okuly Julius _Dodoma

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, anatarajiwa kuzindua Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014, Toleo la 2023 tarehe 31 Januari 2025, jijini Dodoma.

Akizungumza na waandishi wa habari kuelekea uzinduzi huo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, ambaye pia ni Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, amesema kuwa maono ya Rais Dkt. Samia ni kuhakikisha vijana wa Kitanzania wanapomaliza shule wanakuwa na maarifa na ujuzi wa kutosha kwa ajili ya maisha yao na maendeleo ya taifa.

"Lengo la Mheshimiwa Rais ni kuwaandaa wanafunzi kuwa mahiri katika kukabiliana na changamoto za sasa na kuendana na mahitaji ya dunia ya sasa. Mheshimiwa Rais hakupendezwa na hali ya kuwa na wahitimu wa madaraja ya juu wasio na ujuzi wa uzalishaji, hali ambayo huwasababishia changamoto za ajira na maisha," amesema Msigwa.

Ameongeza kuwa kutokana na maono hayo, Mheshimiwa Rais alitoa maelekezo kwa serikali kuhakikisha elimu inalenga kuwajengea wanafunzi maarifa, mwelekeo chanya, maadili na ujuzi unaokidhi mahitaji ya kitaifa na kimataifa, ili waweze kushindana katika soko la ajira duniani.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Carolyne Nombo, amesema kuwa maandalizi ya Sera pamoja na mkakati wa utekelezaji wake yamekamilika.

"Kama mnavyofahamu, Sera inatoa mwongozo wa uendeshaji na utolewaji wa elimu nchini. Mbali na Sera, tumeandaa pia mkakati wa utekelezaji, ambao utawezesha kufanikisha malengo yake," amesema Prof. Nombo.

Ameeleza kuwa Sera hiyo imeelekeza kuboresha mitaala ya elimu kuanzia ngazi ya awali, shule za msingi, sekondari, mafunzo ya ualimu na vyuo vikuu, ili kuhakikisha elimu inayotolewa inawapa wahitimu ujuzi unaohitajika katika soko la ajira na maisha kwa ujumla.

Uzinduzi wa Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014, Toleo la 2023 unatarajiwa kuwa hatua muhimu katika mageuzi ya elimu nchini, ukilenga kuleta mabadiliko chanya kwa kizazi cha sasa na kijacho.


No comments:

Post a Comment