
Na Okuly Julius _DODOMA
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI Mhe. Mohamed Mchengerwa amemuagiza Katibu Mkuu wa Ofisi hiyo kuhakikisha kuhakikisha Muswada wa Sheria ya Usimamizi na Uendelezaji wa Makao Makuu Dodoma unawasilishwa bungeni kabla ya kuvunjwa kwa Bunge la 12 mwaka huu.
Mchengerwa ametoa maagizo hayo Jijini Dodoma katika hafla ya utiaji wa saini Mkataba wa ujenzi wa Soko kuu la Majengo na ujenzi wa kituo cha daladala eneo la Mshikamano, Kizota na Nzuguni
"tutapeleka hati ya dharura bungeni ili kuhakikisha Muswada huu unapelekwa Bungeni ili uweze kujadiliwa na kupitishwa kabla Bunge hili halijavunjwa," amesisitiza Mchengerwa
Pia Mchengerwa amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Dodoma kushirikiana na TARURA pamoja na wizara ya Uchukuzi kuhakikisha wanaboresha miundombinu ya kuingia na kutoka katika Stesheni ya Treni ya Mwendokasi (SGR) Dodoma ili wasafiri wasipate tabu wakati wa kuingia na kutoka.
Aidha, Mchengerwa amemtaka Mkurugenzi Mtendaji wa TARURA kutowapa Zabuni wakandarasi ambao hawatekeleza miradi badala yake ahakikishe wamekamilisha miradi yote ili ikawasaidie wananchi.
"asitokee mkandarasi ambaye hajakamilisha Mradi atakayepewa mradi mwingine ndani ya TARURA nchi nzima maana kuna wakandarasi Wana miradi mingi na hawajaikamilisha sasa maelekezo yangu sitaki kuona mkandarasi akipataka kazi nyingine wakati Ana kiporo hajakikamilisha, "ameeleza Mchengerwa
Kwa upande wake Mbunge wa Dodoma Mjini na Waziri wa Madini Anthony Mavunde amesema hawalizishwi na namna mkandarasi anayetekeleza mradi huo awamu ya kwanza anavyofanya kazi kwani hawatendei haki na tayari fedha kiasi cha Bilioni 24 amekabidiwa kwaajili ya utekelezaji.
"Anatakiwa akabidhi mradi huu Februari 19 mpaka leo ukimuuliza asilimia alizozifikia ameshindwa kufika hata 50% katika baadhi ya maeneo Barabara ya kutoka Mkalama kwenda Ntyuka hajakwenda kwa kasi tuliyoitegemea,"amesema.

Awali akitoa taarifa ya utekelezaji wa miradi ya TACTIC katika Jiji la Dodoma Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA), Mhandisi Victor Seff amesema kuwa mradi unatekelezwa kwa awamu mbili katika Halmashauri zote 12 ikiwemo Jiji la Dodoma.
"Awamu ya kwanza utekelezaji ulianza na Barabara na Mifereji ya maji ya mvua ambapo Mikataba ilisainiwa kwa pamoja tarehe 23/09/2023 na Makandarasi walianza utekelezaji tarehe 20/11/2023 kwa mikataba ya Miezi 15 ambapo imepangwa miradi kukamilika ifikapo tarehe 19/02/2025,"amesema.
Amesema Miradi inayoendelea ya awamu ya kwanza ni ujenzi wa Barabara kwa kiwango cha lami kilomita 10.21, Mtaro wa maji ya Mvua Ilazo kilomita 2.1, Uboreshaji wa Mabwawa ya kuhifadhi maji ya mvua (3) na mitaro ya kutiririsha maji Kilomita 2.81 na ujenzi wa jengo la usimamizi na uratibu wa miradi.
"Katika Jiji la Dodoma, miradi itakayotekelezwa awamu ya 2 ya kundi la kwanza ni uboreshaji wa Soko kuu la Majengo pamoja na kituo cha daladala eneo la Mshikamano, uboreshaji wa Stendi ya mabasi madogo eneo la Kizota, ujenzi wa Stendi ya mabasi madogo eneo la Nzuguni na ujenzi wa Vivuko vya Maji (Footbridges) katika maeneo ya Chaduru, Maili Mbili na Ntyuka,"amesema.




No comments:
Post a Comment