TNCM YAFANYA KIKAO NA WADAU KUJADILI AFUA ZA AFYA NCHINI - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Friday, February 14, 2025

TNCM YAFANYA KIKAO NA WADAU KUJADILI AFUA ZA AFYA NCHINI


Na Mwandishi wetu - Dar es salaam


Tanzania National Coordinating Mechanism (TNCM) imefanya kikao muhimu na wadau mbalimbali wa sekta ya afya ili kujadili maendeleo na changamoto katika utekelezaji wa afua za afya nchini.

Kikao hicho kimefanyika tarehe 13 Februari ,2025 katika Ukumbi wa Mikutano wa Ofisi ya Waziri Mkuu, jijini Dar es Salaam, kikiongozwa na Dkt. Jim Yonazi, Katibu Mkuu (Ofisi ya Waziri Mkuu – Sera, Bunge na Uratibu).

Akizungumza baada ya kikao hicho, Dkt. Yonazi amesema kuwa mkutano huo umejikita katika kutathmini utekelezaji wa afua za afya, ikiwemo mapambano dhidi ya UKIMWI, Kifua Kikuu (TB), na upatikanaji wa vifaa kinga muhimu. 


“Tumejadili hali halisi ya huduma za afya nchini na kushukuru kwamba wadau mbalimbali bado wanaendelea kuiunga mkono serikali. Serikali nayo inaendelea kuwekeza kwa dhati katika afya za wananchi wake,” alisema Dkt. Yonazi.

Kikao hicho pia kimeangazia mbinu za kuhakikisha upatikanaji wa dawa, vifaa tiba, na huduma muhimu kwa wananchi. Wadau wa sekta ya afya wameeleza umuhimu wa ushirikiano kati ya serikali na sekta binafsi katika kuimarisha huduma za kinga na matibabu, huku wakibainisha changamoto zinazohitaji ufumbuzi wa haraka.
 Dkt. Yonazi, aliendelea kwa kusisitiza juhudi za pamoja kati ya serikali na wadau wa maendeleo akisema zinapaswa kuendelea ili kuhakikisha huduma za afya zinaboreshwa kwa manufaa ya wananchi wote.
 
“Tumejadili kwa pamoja namna tunavyoweza kuhakikisha watu wetu wanapata dawa, wanapata kinga, na afua mbalimbali zinazohusiana na upatikanaji wa huduma za afya zinaendelea kutekelezwa kwa ufanisi,” Alisisitiza.

Aidha Tanzania National Coordinating Mechanism (TNCM) ni chombo cha kitaifa kinachoratibu miradi ya afya inayofadhiliwa na Global Fund, kikiwa na jukumu la kuhakikisha rasilimali zinatumika kwa ufanisi katika mapambano dhidi ya UKIMWI, Kifua Kikuu (TB), na Malaria.

No comments:

Post a Comment