AUWSA YAFIKISHA ASILIMIA 99 UPATIKANAJI WA MAJI SAFI JIJI LA ARUSHA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Friday, March 14, 2025

AUWSA YAFIKISHA ASILIMIA 99 UPATIKANAJI WA MAJI SAFI JIJI LA ARUSHA


Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Jiji la Arusha (AUWSA), Mhandisi Justine G. Rujomba, akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio na mwelekeo wa ofisi hiyo katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita, leo Machi 14, 2025, katika Ofisi za Idara ya Habari - MAELEZO, jijini Dodoma.


Na Okuly Julius _ DODOMA


Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Jiji la Arusha (AUWSA) Mhandisi Justine Rujomba amesema, katika mwaka wa fedha 2024/25, upatikanaji wa maji safi umefikia asilimia 99 jijini Arusha, huku mtandao wa majitaka ukipanuliwa kutoka asilimia 8.03 mwaka 2020/21 hadi asilimia 39.5 mwaka huu.

Mhandisi RUJOMBA, ameyasema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio na mwelekeo wa Mamlaka hiyo katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita, leo Machi 14, 2025, katika Ofisi za Idara ya Habari - MAELEZO, jijini Dodoma.

"ili kuwahudumia wananchi ambao hawajafikiwa na mtandao wa majitaka, AUWSA imenunua magari manne ya kunyonya majitaka (Cesspit Emptier Trucks), yenye uwezo wa kubeba lita 5,000 na 10,000. Majitaka yanayokusanywa kutoka kwa wateja zaidi ya 10,930 yanatibiwa katika mabwawa ya kutibu majitaka yaliyopo Terrat (Themi Holding Ground) ambapo majitaka hayo yaliyotibiwa yanawanufaisha wananchi walipo kusini mwa mabwawa hayo kwa kutumia maji hayo yaliyotibiwa kwa shughuli za kiuchumi hususani kilimo cha umwagiliaji"

Na kuongeza kuwa "Tumejipanga kuhakikisha kila mwananchi wa Arusha anapata huduma ya majisafi na usafi wa mazingira kwa kiwango cha juu. Miradi tuliyoitekeleza, kama ule wa Mlangarini na Mirerani, ni hatua muhimu katika kufanikisha malengo yetu." amesema Mhandisi Rujomba

Aidha, amesema kupitia ufadhili wa Serikali ya Tanzania na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), AUWSA imekamilisha mradi mkubwa wa maji wenye thamani ya TZS bilioni 520.

" Mradi huu umejumuisha uchimbaji wa visima virefu, ujenzi wa mtambo wa kutibu maji, na upanuzi wa mtandao wa majisafi na majitaka. Pia, mamlaka hiyo imenunua magari manne ya kunyonya majitaka ili kuwahudumia wananchi ambao hawajafikiwa na mtandao wa maji taka, amefafanua Mhandisi Rujomba

Mhandisi Rujomba ameeleza kuwa, katika bajeti ya mwaka 2025/26, AUWSA inalenga kuendelea kupunguza upotevu wa maji, kuongeza wateja wapya, na kuboresha huduma kwa wateja kwa kutumia teknolojia za kisasa.

"Tunafanya kazi kwa bidii kuhakikisha huduma zetu zinaendelea kuwa bora na kuwafikia wananchi wote," ameongeza Mkurugenzi huyo.

AUWSA inaendelea kutekeleza azma ya kufanikisha malengo ya maendeleo endelevu (SDG 6) ya upatikanaji wa maji safi kwa wote, huku ikishirikiana na wadau wa ndani na wa kimataifa kuboresha zaidi huduma zake.

No comments:

Post a Comment