
Baadhi ya wajasiriamali na wananchi kutoka Kata ya Bugogwa na Busweru Wilaya ya Ilemela, mkoani Mwanza, wakiwa katika Ukumbi wa Halmashauri ya Ilemela pamoja na Timu ya Wataalamu wa Elimu ya Fedha kutoka Wizara ya Fedha na Taasisi zake Wilayani humo, wakichangia mada mbalimbali kuhusu elimu ya fedha waliyoipata kupitia njia ya filamu yenye maudhui kuhusu matumizi sahihi ya fedha, umuhimu wa kupanga bajeti na kuitekeleza, umuhimu wa kusajili vikundi vya huduma ndogo za fedha , utunzaji wa fedha binafsi, umuhimu wa kushirikisha familia na watu wa karibu kwenye masuala ya fedha na uwekezaji, umuhimu wa kukata bima ya biashara na mali nyingine.
(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini-WF, Mwanza)
Na Chedaiwe Msuya, WF, Mwanza.
Serikali kupitia Wizara ya Fedha inaendelea kutoa elimu ya fedha kwa wananchi wa kada zote ili kuwajengea uelewa kuhusu usimamizi bora wa fedha.
Zoezi hilo ni sehemu ya utekelezaji wa Mpango Mkuu wa Maendeleo ya Sekta ya Fedha unaolenga kuimarisha ustawi wa kifedha kwa miaka 2021/2022 hadi 2029/2030.
Mpaka sasa, programu hii imefikia mikoa 16 nchini, ikiwemo Kagera, Singida, Manyara, Kilimanjaro, Arusha, Kigoma, Pwani, Morogoro, Rukwa, Lindi, Mtwara, Tabora, Shinyanga, Simiyu, Mara, na Mwanza. Wakazi wa mikoa hiyo wamepata fursa ya kujifunza mbinu za kuboresha maisha yao kupitia matumizi sahihi ya rasilimali za kifedha.
Katika utekelezaji wa mpango huu, Wizara ya Fedha inashirikiana na taasisi mbalimbali za serikali kama Kampuni ya Uwekezaji ya UTT AMIS, Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA), na Bodi ya Bima ya Amana (DIB). Ushirikiano huu unalenga kuongeza ufanisi katika utoaji wa maarifa kuhusu uwekezaji, akiba, na usalama wa fedha.
Aidha, benki mbalimbali nchini zimejitokeza kusaidia juhudi hizi kwa kutoa elimu kuhusu huduma za kifedha. Benki Kuu ya Tanzania (BoT), pamoja na benki za biashara kama TCB, NMB, CRDB, na NBC, zimekuwa zikishiriki katika mafunzo na semina mbalimbali zinazolenga kuwawezesha wananchi kusimamia fedha zao vyema.
Kwa kupitia Elimu ya Fedha, wananchi wanapata uelewa kuhusu umuhimu wa kupanga bajeti, kujiunga na vikundi vya kifedha, na kulinda mali zao kwa kukata bima. Wizara ya Fedha inaendelea kusisitiza kuwa elimu ya fedha ni nyenzo muhimu katika kuinua uchumi wa mtu binafsi na taifa kwa ujumla.




No comments:
Post a Comment