Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu imeisisitiza Wizara ya Ujenzi kuendelea na mkakati wa kuinua na kuwasaidia Makandarasi wazawa ili kuwajengea uwezo katika utekelezaji wa miradi ya mbalimbali ya ujenzi nchini.
Hayo yameelezwa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Selemani Kakoso leo Januari 21, 2026 mara baada ya kupokea taarifa ya Wizara ya Ujenzi kuhusu muundo, majukumu pamoja na Sera na Sheria zinazotekelezwa na Wizara hiyo iliyowasilishwa na Waziri wa Ujenzi, Mhe. Abdallah Ulega mbele ya kamati hiyo Bungeni jijini Dodoma.
"Wekeni mazingira mazuri ya kuwasaidia makandarasi wa ndani, ongezen fursa mbalimbali za miradi, walipwe kwa wakati kwani mkifanya hivi mtasaidia ufanikishaji wa utekelezaji wa miradi ya ujenzi nchini na kusaidia kukuza uchumi wa nchi", amesema Kakoso.
Aidha, Kakoso ametoa rai kwa Wizara hiyo kutekeleza miradi ya ujenzi kwa kushirikiana na Sekta Binafsi (PPP) ili Wizara kupata wigo na fursa ya kutekeleza miradi mingi zaidi kupitia mfumo huo.
Kwa upande wake, Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega ameeleza mafanikio ya Wizara hiyo kwa Kamati katika kipindi cha miaka mitano ambapo amesema kuwa mtandao wa barabara umeongezeka kutoka kilometa 36,361.95 mwaka 2020 hadi kilometa 37,435.04 mwaka 2025 huku
barabara zenye urefu wa kilometa 5,769.74 zikiwa katika hatua mbalimbali za utekelezaji.
Ameongeza kuwa Wizara imekamilisha ujenzi wa madaraja makubwa nane (8) ambapo ameyataja madaraja hayo kuwa ni Daraja la J.P Magufuli (Mwanza), Tanzanite (Dar es Salaam), Msingi (Singida), Wami (Pwani), Kitengule (Kagera), Ruhuhu (Ruvuma), Kiyegeya (Morogoro) na Gerezani (Dar es Salaam).
Ulega ameeleza kuwa Wizara inaendelea na utekelezaji wa miradi inayolenga kuondoa changamoto ya msongamano wa magari mijini ikiwemo ujenzi wa miundombinu ya mabasi yaendayo haraka (BRT) Awamu ya 3 na 5, ujenzi wa barabara ya mzunguko wa ndani jijini Dodoma (km 6.3) ujenzi wa barabara ya mchepuo wa Iringa (km 7.3) na ukamilishaji wa ujenzi wa barabara ya mzunguko wa nje katika jiji la Dodoma (km 112.3).
Miradi mingine ni upanuzi wa barabara ya Uyole - Ifisi - Songwe Airport (km 29), upanuzi wa barabara ya Arusha - Holili, sehemu za Tengeru -Usa River (km 11.7), Maili Sita - Kiboroloni (km 11.7) na Daraja la Kikafu (m 560).









No comments:
Post a Comment