
Waziri wa Nishati, Mhe. Deogratius Ndejembi, akizungumza katika kikao
na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kilichofanyika
katika Kumbi za Bunge Jijini Dodoma.Kikao hicho kilihusu uwasilishaji
wa taarifa kutoka Wakala wa Nishati Vijijini (REA) na Shirika la umeme
Tanzania (TANESCO) kuhusu muundo na majukumu ya taasisi hizo. Kushoto
kwa Waziri ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi
Mramba na kulia kwake ni Mkurugenzi Mkuu wa REA Mhandisi Hassan Saidy.

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Mhe. Subira Mgalu akizungumza katika kikao kati ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini na Menejimenti ya Wizara ya Nishati nataasisi zake. Kikao hicho kilihusu uwasilishaji wa taarifa kutoka Wakala wa Nishati Vijijini (REA) na Shirika la umeme Tanzania (TANESCO) kuhusu muundo na majukumu ya taasisi hizo.
Na Mwandishi Wetu, Dodoma
Licha ya kuongezeka kwa gharama za vifaa vya umeme ikiwemo nguzo, waya
na mita, Serikali imeendelea kuhakikisha gharama za matumizi ya umeme
kwa wananchi hazipandi kwa kipindi cha miaka 10 kuanzia mwaka 2016.
Akizungumza Januari 21, 2026 jijini Dodoma katika kikao cha pili kati
ya Wizara ya Nishati, taasisi zake na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya
Nishati na Madini, Waziri wa Nishati, Mhe. Deogratius Ndejembi,
amesema hatua hiyo imelenga kila mwananchi apate huduma ya umeme kwa gharama nafuu.
Amesema kiwango cha uunganishaji wa umeme nchini kimefikia asilimia
52, huku Serikali ya Awamu ya Sita ikiweka lengo la kufikia asilimia
75 ifikapo mwaka 2030 linalotekelezwa kupitia Mpango wa Nishati
uliosainiwa Januari 2025 wakati wa Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Afrika.
Akizungumzia suala la mita janja, Waziri Ndejembi amesema kuwa zoezi
la uunganishaji wa mita hizo linaendelea nchi nzima na zitamwezesha
mwananchi kupata umeme mara moja baada ya kununua token bila kutumia
kifaa cha ziada cha kuingiza namba (CIU), hatua itakayopunguza
changamoto zilizokuwepo katika mfumo wa awali.
Kuhusu upatikanaji wa umeme wa Gridi mkoani Rukwa, Waziri Ndejembi
amesema mradi wa njia ya kusafirisha umeme wa kilovoti 400 unaendelea
kutekelezwa kupitia mkandarasi TBEA na itawezesha mkoa huo kupata
umeme wa uhakika na wa kuaminika.
Aidha, ametaja mradi wa kuimarisha upatikanaji wa umeme katika mikoa
ya Mtwara, Lindi, Tabora na Simiyu, unaotekelezwa na mkandarasi
Kalpataru.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Mhe. Subira Mgalu, amepongeza Shirika la Umeme Tanzania
(TANESCO) na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kwa kazi kubwa wanayoifanya katika kuhakikisha wananchi wanapata nishati ya umeme ya uhakika.
Amesema mafanikio hayo yametokana na maono ya Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kupitia
utekelezaji wa miradi mikubwa ya uzalishaji umeme ikiwemo Mradi wa
Julius Nyerere (JNHPP) wa megawati 2,115, mradi wa umeme wa jua wa
Kishapu unaotarajiwa kuanza kuzalisha megawati 50, pamoja na mradi wa
Malagarasi wa megawati 49 unaoendelea kutekelezwa.
Mhe. Mgalu ameongeza kuwa kuimarika kwa upatikanaji wa umeme
kumechangia kwa kiasi kikubwa ukuaji wa uchumi na ongezeko la mapato
ya Serikali, hususan katika sekta za viwanda na migodi, hali iliyoisaidia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuvunja rekodi ya
makusanyo kwa kufikia Sh.trilioni 4.13 mwezi uliopita.
Vilevile, amepongeza REA kwa kuwapa kipaumbele wakandarasi wa ndani
katika miradi ya usambazaji umeme pamoja na kampeni ya kuhamasisha
matumizi ya nishati safi ya kupikia, akisisitiza umuhimu wa elimu hiyo
kufika hadi ngazi ya shule za awali.

No comments:
Post a Comment