OR-TAMISEMI
Mkurugenzi wa Idara ya Usimamizi wa Elimu, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Dkt. Emmanuel Shindika, amewataka Maafisa Elimu wa Mikoa na Halmashauri kuhakikisha wanaimarisha ufuatiliaji na usimamizi wa elimu katika maeneo yao ili kuleta mabadiliko chanya kwenye Sekta ya Elimu nchini.
Dkt. Shindika ametoa wito huo leo Machi 7, 2025 alipokuwa akifunga Mkutano Mkuu wa Umoja wa Maafisa Elimu wa Mikoa na Halmashauri (REDEOA), uliofanyika Jijini Dar es Salaam ambao unatathmini utekelezaji wa shughuli za elimu kwa kipindo cha kuanzia mwezi Julai hadi Desemba, 2024.
Amesema ni muhimu kuimarisha usimamizi wa elimu kwa kuhakikisha uandikishaji wa wanafunzi wa shule za awali na msingi unasimamiwa kwa ukaribu ili kufanikisha malengo ya serikali katika Sekta ya Elimu.
"Uandikishaji wa wanafunzi wa awali na msingi bado ni changamoto katika maeneo yenu. Hakikisheni mnasimamia kwa karibu suala hili ili kutimiza malengo yaliyowekwa na Serikali," amesisitiza.
Pia amewataka Maafisa Elimu kusikiliza na kutatua changamoto zinazowakabili walimu ili kuongeza tija na ufanisi katika ufundishaji na kuimarisha mahusiano mazuri kazini, kuwalipa walimu stahiki zao kwa wakati, na kuhakikisha malipo ya likizo hayacheleweshwi.
Aidha, amewaelekeza Viongozi hao kusimamia kwa weledi utekelezaji wa miradi ya elimu katika maeneo yao, ili ikamilike kwa wakati na kuendana na thamani ya fedha iliyotengwa huku akisisitiza ushirikiano wa karibu kati ya Maafisa Elimu na Wadau mbalimbali wa elimu ili kuimarisha ubora wa elimu nchini.
No comments:
Post a Comment