
Mkurugenzi Mkuu Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), CPA. Anthony Kasore. akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio na mwelekeo wa mamlaka hiyo katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya awamu ya sita tarehe 3 Machi, 2025, katika ofisi za Idara ya Habari - MAELEZO, Dodoma.
Na Okuly Julius _DODOMA
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) , CPA. ANTHONY MZEE KASORE, amesmea katika kipindi cha mwaka 2021 hadi 2024, Serikali imekamilisha ujenzi wa vyuo 33 vya ufundi stadi, 29 vikiwa vya wilaya na vinne (4) vya Mkoa, kwa gharama ya Shilingi Bilioni 94.5.
Amesema Serikali ilitenga Shilingi Bilioni 103 kwa mwaka wa fedha 2022/2023 kwa ajili ya ujenzi wa vyuo vipya 64 vya Wilaya na kimoja cha Mkoa wa Songwe, ambavyo vitachangia ongezeko la udahili wa wanafunzi 89,700.
Akitoa taarifa ya mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Sita katika kipindi cha miaka minne ndani ya Taasisi hiyo, CPA KASORE amesema, kwa sasa, VETA ina vyuo 80, mwishoni mwa mwaka h
(2025) vyuo vinavyojengwa vinatarajiwa kukamlika, hivyo tutakuwa na vyuo 145.
"Serikali kupitia VETA imefanya upanuzi wa miundombinu ya kutolea elimu na mafunzo ya ufundi stadi nchini kwa kutoa fedha ili kuongeza majengo mapya na ukarabati wa majengo ya zamani ili kuweka mazingira wezeshi ya kukuza ubora wa mafunzo na kuongeza fursa za udahili katika vyuo vya VETA,
Na kuongeza kuwa "Katika eneo hili katika kipindi cha miaka minne, Serikali imetoa kiasi cha shilingi bilioni 14.2, ambazo zimewezesha uboreshaji na upanuzi wa miundombinu ya vyuo vya Newala, Ngorongoro, Moshi, Dar es Salaam (Changombe), Kipawa, Mtwara, Mwanza, Mikumi, Karagwe, Chuo cha Ualimu wa Ufundi Stadi Morogoro (MVTTC) Kihonda, Nkasi, Nyamidaho, Kanadi, Ileje, Namtumbo, Mabalanga, Gorowa, Arusha na Busokelo, " amesema CPA KASORE
Katika Hatua nyingine CPA. Kasore amesema kuwa, VETA itaendelea kusimamia na kuboresha utoaji wa mafunzo ili kuhakikisha Watanzania wengi zaidi wanapata ujuzi na kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo ya Taifa, hatimaye kutimiza maono ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ya kutoa elimu ujuzi kulingana na mazingira ya nchi na soko la ajira pamoja na Dira yetu ya 'Tanzania yenye Mafundi Stadi Mahiri na wa Kutosha.
”Masuala mengine ni ubiasharishaji wa huduma za Mamlaka kupitia Kampuni Tanzu, kuimarisha ushirikiano na Vyuo vya nchi nyingine na Wabia wa Maendeleo, kufanya Tathmini ya Mahitaji ya Ujuzi kwenye maeneo mbalimbali nchini, kuadhimisha miaka 30 ya VETA pamoja na miaka 50 ya Ufundi Stadi”, amesema CPA. Kasore.
Amefafanua kuwa, kutokana na kupanuka kwa fursa na uwekezaji mkubwa unaoendelea kufanywa na Serikali katika nyanja mbalimbali, makampuni mengi yakiwemo ya kigeni yanahitaji mafundi wenye ujuzi unaokubalika kimataifa hivyo VETA imeandaa mkakati na kuanza kutekeleza kutoa mafunzo yanayoelekea kwenye tunuku za kimataifa (International Certification).
“Tutafanya hivyo kupitia Vituo vya Umahiri (Centres of Excellence) ambapo tumepanga kuwa na vituo 14 vya umahiri nchini kote. Kwa sasa, tumefanya ununuzi wa vifaa vya kisasa vya Fani ya Uchomeleaji na Uungaji Vyuma vyenye gharama ya Shilingi bilioni 1.773 vikihusisha Welding Simulators kwa Vyuo vya Moshi RVTSC na Dodoma RVTSC.
Vile vile, VETA inashirikiana na Makampuni na waajiri zaidi ya 100 kwa ajili ya kutoa mafunzo ya vitendo mahali pa kazi, taasisi imepanga kupanua zaidi mafunzo kwa mfumo rasmi wa uanagenzi kwa kushirikiana na viwanda. Aidha, VETA imeanzisha mpango wa VETA na Fundi Mahiri ambapo wanashirikiana kutoa mafunzo na shughuli za uzalishaji.
Pia, VETA imepanga kuufanya utunuku kwenye mafunzo ya ufundi stadi kuwa nyumbufu ili kuruhusu wanafunzi wa kozi za muda mfupi kujikusanyia masaa kwa mahairi zilizopatikana na hatimaye kupata tunuku za kitaifa katika ngazi za ufundi stadi. VETA imeanzisha kampuni ya ambayo itakuwa ikifanya kazi za kubiasharisha ubunifu, bidhaa na huduma za VETA lengo la kuanzisha Kampuni Tanzu ni kuongeza uzalishaji wa ndani na kupunguza utegemezi wa ruzuku kutoka Serikalini.
Kupitia ushirikiano na vyuo vya nje, CPA Kasore amesema mpango huo unalenga kubadilishana uzoefu na kujenga uwezo kwa wakufunzi; kupata vifaa vya kisasa vya mafunzo; kukuza mbinu za kisasa za ufundishaji na ujifunzaji ambapo miongoni mwa nchi zitakazoendelea kushirikiana na Tanzania ni pamoja na China, Uingereza, Korea ya Kusini, India, Scotland na Ujerumani. Wabia wa Maendeleo tutakaoendelea kushirikiana nao ni pamoja na GIZ, KOICA, Benki ya Dunia, UNESCO, n.k.
Fauka ya hayo, VETA imeshafanya tathmini ya mahitaji ya ujuzi katika shughuli za kiuchumi na kijamii zinazofanyika kwenye mikoa na wilaya zote nchini hivyo itandelea kufanya ‘Skills Mapping’ kwa lengo la kuhakikisha kuwa ujuzi unaohitajika unatolewa kwenye Vyuo vya vya Ufundi Stadi vilivyopo kwenye Mikoa na Wilaya zote. Aidha, Bodi ya VET pamoja na Menejimenti wanafanyia kazi kanuni za vyuo ili kuwavutia watu wote kwenda VETA kusoma.
VETA imekuwa ni Taasisi muhimu inayochangia rasilimali watu wenye ujuzi wanaohudumu katika sekta mbalimbali ikiwemo viwanda, kilimo, ujenzi, teknolojia, Nishati na huduma na Utalii. Kwa kipindi cha miongo mitatu, VETA imeendelea kuwa mstari wa mbele katika kuwajengea Watanzania uwezo wa kujiajiri, kuajiriwa na kuchangia katika kukuza uchumi wa nchi.

No comments:
Post a Comment